Wednesday 12 December 2012

UNAJUA KUWA SHULE YA KWANZA TANZANIA ILIJENGWA MUHEZA TANGA?

HAYA NI BAADHI YA MAJENGO YALIYOJENGWA KATIKA SHULE HIYO BAADAE.... MWAKA 1848 Mmishenari wa Kijerumani Dk Johan Ludwig Krapf,alitembelea kijiji cha Magila kilichopo Muheza mkoani Tanga akiwa katika safari zake za Afrika Mashariki. Magila kuna mlima ulio katika safu za milima ya Usambara ukipakana na mlima wa Magoroto ambao ndio chanzo cha maji ya mto Mkurumuzi unaoelekea Muheza. Historia inaonyesha eneo la mlima Magila wenye miamba na mawe mengi, zamani kabla ya kuja wageni lilitumika kuwatenga wagonjwa wa ukoma na magonjwa mengine yasiyotibika, kwa lengo la kuwazuia wasiwaambukize wengine. Dk Krapf alipofika na kuwaona wagonjwa hao waliokuwa wakiishi kwa madhila makubwa, alichonga msalaba katika mti wa mkuyu kwa imani kuwa Mwenyezi Mungu angewaponya wagonjwa hao. Eneo hilo ndilo lililokuja kujengwa shule ya kwanza na Waingereza mwaka 1886. Alama ya msalaba huo ipo hadi na sasa na ndipo ilipo Shule ya Sekondari Hegongo. Hadi leo mahali hapo panaitwa Magila Msalabani. Kwa sasa Magila ni kata yenye vijiji vya vya Magila, Mikwamba, Misongeni na Mafleta. Mkaazi wa eneo hilo Luteni Kanali mstaafu John Mhina amekamilisha kuandika kitabu kuhusu historia ya Magila Msalabani,kinachoeleza historia ya kijiji hicho na ujio wa wazungu walioanzisha shule ya kwanza Tanganyika na kanisa. Luteni Kanali Mhina aliyelitumikia Taifa kwa muda mrefu kama mwanajeshi, na baadaye kuwa Mbunge wa Muheza kutoka mwaka 1990 hadi 1995,anasema harakati za kuanzisha shule katika kijiji hicho zilitokana na Wamishenari waliokuja Afrika Mashariki kutoka Ulaya kwaajili ya kueneza dini ya kikristo tangu miaka ya 1770. Anawataja baadhi ya Wamishenari hao kuwa ni pamoja na David Livingstone,Charles Mackenzie, William Tozer na Edward Steer. Anasema harakati hizo zilianzia tangu visiwa vya Zanzibar mwaka 1863 ambako pia walikomesha biashara ya utumwa na kuanza ujenzi wa kanisa la Anglikana la Mkunazini Zanzibar kwa miaka 10 tangu mwaka 1873. Anasema wakati huo kulikuwa na shule iliyoanzishwa Zanzibar maeneo ya Kiungani na Kiinua mguu na Askofu William Tozer mwaka 1869. Hata hivyo, anasema shule hiyo haikuwa rasmi na ilikuwa ikifundisha elimu ya dini kwa watumwa waliokombolewa.

0 comments:

Post a Comment