Tuesday 17 April 2012

Umuhimu wa matumizi ya chumvi kwa Binadamu

CHUMVI ni aina ya madini yenye umuhimu na faida nyingi, kwa mtumiaji, ikiwa atatumia kwa kiasi kinachotakiwa kwenye mlo wake. 

Kwa maisha ya kawaida, huwezi kukosa madini hayo au kiungo hicho kwenye familia mbalimbali, mara nyingi utaikuta jikoni au hata mezani. Chumvi pamoja na muonekano 
wake ni kiungo au madini ambayo hupatikana kwa urahisi na bei nafuu kuliko viungo vingine vya chakula au madini duniani. 

Pamoja na umuhimu wake, lakini si rahisi ukasikia kesi au masuala ya chumvi kuibwa kama zilivyo bidhaa nyingine kwenye maduka mbalimbali. Mfano mdogo ni kiungo kama mafuta ya kula, hiyo ni bidhaa ambayo ukiiweka pamoja na chumvi, ukamwambia mtu achague bidhaa 
moja aondoke nayo, wengi watachagua mafuta. 

Lakini jamii inapaswa kufahamu kwamba, katika afya ya mwanadamu au hata mnyama chumvi ina umuhimu mkubwa, ingawa wengi wetu tunaona ni kiungo cha kawaida sana. Ni miaka mingi sasa chumvi (chloride), inatumika kuhifadhi vyakula, kuongeza ladha kwenye chakula na mara nyingine hutumika kusafisha vitu. 

Kwa kawaida chumvi ni madini au tunaweza kuita rasilimali isiyoisha, ambayo hupatikana kwa urahisi na ili ifae kwa matumizi ya binadamu huhitaji kuongezwa madini joto. 

Chumvi huzalishwa kwa njia mbalimbali, kuna chumvi iliyotengenezwa mahususi kwa ajili ya matumizi ya jikoni, mezani na pia ipo chumvi iliyoongezwa madini ya chuma ambayo ndiyo inayotumika kwa wingi katika jamii. 

Kwa wale wasiofahamu manufaa ya chumvi na matumizi yake ni vyema wafahamu na kuchukua hatua kwani matumizi ya chumvi pia ni tiba kwa baadhi ya maradhi na pia hupunguza kero zitokanazo na kuumwa na wadudu mbalimbali. 

Kwa matumizi jikoni Mbali na kutumika kwenye maabara kwa kuhifadhi vyakula, kuoka, chumvi hutumika jikoni kwa kuongeza ladha kwenye vyakula mbalimbali vipikwavyo. 
Pia chumvi hutumika kuchunguza iwapo mayai ya kuku au bata kama ni mabovu au mazima. 

Katika upimaji huo, tumia kijiko cha chai kupima, ambapo weka chumvi vijiko viwili, changanya na maji kwenye bakuli au chombo, kisha tumbukiza yai moja baada ya jingine. 

Ikiwa yai ni bovu litaelea juu ya maji na kama ni bovu au lina muda mrefu tangu litagwe na kuku au bata litazama kwa kuwa kiwango cha hewa ndani ya seli ya yai huongezeka kadri yai linapokaa muda mrefu baada ya kutagwa. 

Hata hivyo kama yai limeelea huenda sio bovu ila limekaa muda mrefu baada ya kutagwa na njia muafaka wa kubaini baada ya kulipima kwa njia ya chumvi ni kulipasua na kuona ndani kuna nini. Kadhalika yai kama ni zima litazama hadi chini kwenye chombo husika. 

Kuhifadhi matunda yasiharibike rangi Matunda mengi duniani kama vile tufaa na peas huhifadhiwa kwa kutumia limau au siki kufanya matunda hayo yasibadilike rangi na kuwa ya udhurungi au kahawia. 

Lakini chumvi nayo hutumika kwenye kazi hiyohiyo kwani sio wote wenye uwezo wa kununua siki au malimau ya kutosha kuhifadhi matunda, ila kiasi kidogo tu cha chumvi kilichochanganywa na maji hufanya matunda kuwa katika rangi yake ya kawaida kwa muda mrefu. 

Usafi wa kinywa Chumvi hutumika pia kufanya mswaki wako udumu muda mrefu. Kabla ya kutumia mswaki mpya chukua kiasi kidogo cha chumvi changanya na maji kisha tumbukiza mswaki kwa muda kidogo halafu utoe. 

Njia hiyo hufanya mswaki kudumu muda mrefu bila kuharibika, kukakamaa au kutengeneza umbo kama ua lililochanua. Kadhalika chumvi hutumika kusafisha meno, ambapo kiasi kidogo 
cha chumvi huwekwa kwenye mswaki na mtumiaji kuswaki ambapo matokeo yake meno hung’aa na kuwa imara. 

Wataalamu wa afya ya kinywa wanasema chumvi ni nzuri pia kwa kutunza kinywa dhidi ya harufu mbaya. Katika jamii wapo baadhi ya watu ambao midomo yao hutoa harufu. Ili kuzuia kero hiyo kiasi cha chumvi pamoja na maji ya uvuguvugu mtumiaji husukutua kinywa na hatimaye kuondoa harufu hiyo mbaya. 

Kuumwa na wadudu Watabibu wanasema chumvi hutumika pia kutibu au kupunguza makali 
ya kuumwa na wadudu kama vile nyuki na wadudu watambaao. Utafiti wa sayansi mbalimbali katika vyuo vya tiba na dawa nchini Marekani, na Uingereza wanasema kiasi cha chumvi husaidia kupunguza maumivu ya kuumwa na nyuki au wadudu wengine. 

Kiasi kidogo cha chumvi huwekwa kwenye eneo lililoumwa na nyuki au wadudu na baada ya muda kidogo, maumivu hupungua kama sio kuisha. Pia kuna baadhi ya watu wakiumwa na mbu hubakia na vipele ambavyo vina maumivu, hivyo wataalamu wanashauri kwamba kiasi cha chumvi kilichochanganywa na mafuta ya mzeituni kitumike kutibu eneo hilo. 

Kadhalika magonjwa ya koo kama vile muwasho wa mafua kiasi cha chumvi ilichochanganywa na maji ya uvuguvugu, mgonjwa akitumia kusukutua, huleta nafuu kwa mgonjwa. Chumvi hutumika pia kufukuza wadudu kama vile sisimizi na siafu nyumbani. 

Kwa wapambaji kwenye maeneo mbalimbali kama vile kumbi za harusi na hata nyumbani, chumvi hutumika kufanya maua yadumu kwa muda mrefu bila kunyauka. Chumvi kiasi huchanganywa kwenye maji katika chombo cha maua na kisha kutumbukiza maua, ambayo 
yatadumu kwa muda mrefu bila kunyauka. 

Hayo ni baadhi tu ya matumizi ya chumvi kiafya na pia katika matumizi mengine, wataalamu wa afya wanashauri kwamba kiasi cha chumvi mwilini ni muhimu kwa afya na uhai wa binadamu. Hata hivyo wataalamu wa afya wanashauri kwamba chumvi itumike vizuri kwani itumikapo vibaya huwa na madhara mbalimbali. 

Madhara hayo hutokana na jinsi chumvi hiyo ilivyotayarishwa yaani kutoka kuchimbwa ardhini hadi kufungashwa tayari kwenda kwa mlaji. 

Mtu akipatwa na shinikizo la damu ana uwezekano mkubwa wa kuwa na magonjwa ya moyo, ambayo ni pamoja na moyo kushindwa kusukuma damu na mengineyo ambayo huweza kusababisha mtu akapatwa na mshtuko wa ghafla wa moyo na kisha akapoteza maisha. 

Jambo hilo limegunduliwa na Watafiti wa masuala ya afya wa vyuo mbalimbali duniani wakiwemo wa Chuo Kikuu cha California, Marekani. Imebaikina kwamba kwa kila binadamu wenye umri mkubwa watatu, mmoja kati yao anasumbuliwa na shinikizo la damu. 

Ushauri wa kitiba unasema ni vyema wanadamu wakapunguza matumizi ya chumvi yasiyo na lazima kwenye vyakula. Inashauriwa kwamba kwa siku moja kiasi cha miligramu 2,400 cha 
chumvi ndicho kinahitajika mwilini na si zaidi. 

Kiasi hicho ni sawa na kijiko cha chai kimoja, na kwa wale wenye tatizo la shinikizo la damu kiasi cha miligramu 1,500 sawa na nusu kijiko cha chai cha chumvi. Mtafiti katika chuo hicho, 
Dk.Kirsten Bibbins-Domingo anasisitiza matumizi sahihi ya chumvi kiasi kwa ajili ya kupunguza uwezekano wa kupata maradhi yanayotokana na shinikizo la damu. 

Kwa wale wanaopenda kula vyakula vilivyokwisha fungashwa ni vyema wakasoma maelekezo na kuona kiasi cha chumvi kilichowekwa, ili kuepuka matumizi mengi ya madini hayo mwilini. 
Anasema chumvi ikitumiwa kwa kiasi haina madhara na pia ni dawa, lakini matumizi mabaya ya madini hayo huleta madhara makubwa kwa afya wa walaji, pasipo wao kufahamu. 

Katika matokeo ya utafiti mmoja kuhusu matumizi ya chumvi kwa binadamu, wanasayansi wa tiba wamebaini kwamba matumizi madogo ya chumvi hupunguza hatari ya kupata magonjwa ya mishipa ya moyo. 

Kila mwaka magonjwa mapya ya moyo zaidi ya 120,000 hujitokeza, wanaopata kiharusi wakiwa zaidi ya 67,000 na mshuko wa moyo wagonjwa zaidi ya 100,000. Wagonjwa hao ni katika pembe mbalimbali za dunia na kwamba matumizi sahihi ya chumvi kwa waliozingatia yamesaidia kupunguza tatizo hilo kwa Bara la Afrika na Amerika. 

Matumizi hayo sahihi wa watu wa mabara hayo mawili yamesaidia kuzuia vifo takribani 92,000 kwa mwaka.

0 comments:

Post a Comment