Tukumbuke kwamba uzima wa mtu unategemea sana kinga aliyonayo mwilini,kinga ambayo hujengwa na ulaji wa vyakula vyenye virutubisho vya aina mbalimbali.
Kwa namna ambavyo Mungu ametuumba, mwili unapaswa kujilindi wenyewe dhidi ya maradhi ya kila aina.
Ukiwa na kinga imara ya mwili siyo rahisi kuugua mara kwa mara.
Magonjwa yanayojitokeza haraka pale kinga ya mwili inapokuwa chini, ni pamoja na kuugua malaria mara kwa mara, kifua kikuu, kutokwa na majipu, kutokwa uvimbe wa ajabuajabu katika mwili, kupatwa na mkanda wa jeshi, kupatwa na saratani na magonjwa mengine ya maambukizi.
Huo ni mfano wa kundi moja la magonjwa ya maambukizi, lakini hata magonjwa mengine hatari kama shinikizo la damu, magonjwa ya moyo, magonjwa ya viungo, kisukari, macho, na mengine mengi, huwa ni matokeao ya ulaji wa vyakula visivyo sahihi au uachaji wa ulaji vyakula muhimu.
CHANZO CHA KUSHUKA KWA KINGA
Ili uwe na kinga imara ya mwili, ni lazima uwe unakula mlo kamili unaojumuisha matunda, mboga za majani, nafaka na vyakula vingine vya asili, kwa sababu kila unachokula kina faida yake mwilini. Lakini siyo tu kula chochote kinachoitwa ‘chakula’, bali ule kilichosahihi na kilichosahihi.
Katika maisha tunayoishi sasa, hasa mijini, idadi Kubwa ya watu hawali kabisa vyakula sahihi, badala yake wanakula vyakula ambavyo si tu ni hatari kwa afya zao, bali pia hudhoofisha kinga ya asili ya mwili na hivyo kuufanya mwili kubaki dhaifu na unaoweza kupatwa na ugonjwa wowote.
Chanzo kikuu cha kushuka kwa kinga ya mwili kunasababishwa na ulaji wa vyakula visivyo sahihi ambavyo ndivyo vinavyopatikana kwa wingi kila mahali, hasa sehemu za mijini. Vyakula visivyofaa ndivyo vinavyotangazwa na kunadiwa kwenye vyombo vya habari kuwa bora.
VYAKULA HATARI VINAVYOLIWA KILA SIKU
Kuna orodha ndefu sana ya vyakula hatari ambayo huliwa kila siku, kuanzia asubuhi hadi jioni.
Vyakula hivi yumkini huliwa kwa takriban maisha yote ya mtu na huonekana ni vya kawaida.Baadhi ya vyakula hivyo ni kama vile unga wa ugali, mkate, chips na juisi.
UNGA WA UGALI
Unga wa ugali unaotumiwa na watu wengi nchini ni sembe nyeupe. Chakula kikuu katika kaya nyingi zinazotumia ugali kama mlo wa kila siku huwa ugali mweupe uliotokana na mahindi yaliyokobolewa na kusafishwa, kisha kusagwa na kutoa unga safi mweupe.
Kwa mtizamo wa macho na ladha ya mdomoni, wengi wanaamini kuwa ugali wa aina hii ndiyo mzuri na unaotakiwa kuliwa.
Ulaji wa ugali wa aina hii hauna faida yoyote mwilini, kwani hauna virutubisho,kwa sababu vilishaondolewa vyote wakati wa kukoboa.
Virutubisho muhimu vya muhindi viko kwenye kiini chake, hivyo unapokiondoa unakuwa umeondoa lishe muhimu. Ndiyo maana hata panya hawali mahindi yaliyokobolewa.
Kwa faida ya afya zetu na kwa ajili ya kuimarisha kinga ya miili yetu, sote tunatakiwa kula ugali wa dona, mtama au ulezi kabla hata ya kuugua. Vyakula hivi ni muhimu sana na siyo vya kimasikini kama ambavyo watu wengi wanadhani. Kwa bahati mbaya, upatikanaji wa unga wa dona umekuwa mgumu na ghali kuliko sembe nyeupe, hivyo kuwafanya watu wengi kukimbilia sembe nyeupe ambayo inapatikana kirahisi kila kona ya nchi na kwa bei nafuu.
Kwangu mimi naliona tatizo hili ni la kitaifa na kisera. Serikali kupitia Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, ilipaswa kutoa elimu ya kutosha ya kuelezea madhara yatokanayo na ulaji wa sembe nyeupe kisha kuweka sera itakayokataza uzalishaji wa kibiashara wa sembe nyeupe kama ilivyo sasa.
Sera ya namna hii ingeokoa maisha na afya za Watanzania wengi wanaoteketea kila situ kutokana na ugonjwa wa kisukari.
Naamini kaya nyingi nchini hazijui kabisa kama ugali utokanao na sembe nyeupe wanaokula kila siku iendayo kwa Mungu, una madhara kiafya.
Ni vigumu kuzieleza na zikakuelewa familia ambazo kwa maisha yao yote zimekuwa zikiamini kwamba kula ugali mweupe ndiyo kitu bora.
Serikali ilipaswa kuliangalia suala hili na kuona kama janga la kitaifa, ilipaswa kuanzisha kampeni maalum ya kutoa elimu kuhusu vyakula na lishe kwa njia mbalimbali, zikiwemo za matangazo redioni na kwenye televisheni.
ULAJI WA MATUNDA NA MBOGA
Hakuna kitu muhimu kwa mwili wa binadamu kama kujenga kinga ya mwili. Mwili unapokuwa na kinga imara, si rahisi kuugua magonjwa ya ajaba. Miongoni mwa kazi nyingi za matunda na mboga za majani, ni pamoja na hiyo kazi ya kujenga mwili na kuujengea uwezo wa kujikinga wenyewe.
Pamoja na umuhimu huo, ni watu wachache sana hula matunda na kuyachukulia kama sehemu ya milo yao ya kila siku. Watu wengi hula matunda au mboga za majani ‘kwa bahati mbaya’, huona siyo chakula muhimu sana.
Hili ni kosa kubwa miongoni mwa makosa mengi yanayofanywa na watu katika masuala ya afya.
Matunda yanatakiwa kuliwa kila siku na kwa wingi, vivyohivyo mboga za majani. Unapoacha kula matunda na mboga za majani za aina mbalimbali, jua unaukosesha mwili wako kinga dhidi ya maradhi yanayoweza kujitokeza mwilini.
VYAKULA HIVI NDIYO VINAVYOTUMALIZA
Vyakula tunavyotakiwa kuvila, hatuvili tena na pengine upatikanaji wake ni wa shida, hivyo tunalazimika kula vilivyopo licha ya kuwa vina madhara kwa afya zetu. Hali hii imeongeza idadi ya wagonjwa na magonjwa sugu.
Chakula kikuu cha mijini ni chips, kuku, mayai, soda, juisi za makopo au paketi, nyama choma na pombe. Pia kuna mkate mweupe, maandazi na chapati. Vyakula hivi huliwa kila siku, lakini ukivichambua utagundua havina faida yoyote mwilini zaidi ya kuingia na kutengeneza maradhi.
CHIPS
Chips ambayo kwa kawaida hutengenezwa kutokana na viazi mviringo na kukaangwa kwenye mafuta, ni chakula kinachotakiwa kuliwa kwa kiasi kidogo na kwa nadra sana, kwa sababu kiko kwenye kundi la vyakula vyenye mafuta mengi ambavyo huliwa kwa uchache sana.Lakini hali halisi ni kinyume chake.
KUKU
Kwa kawaida, kuku wengi wanaotumika kwenye biashara ni kuku wa kizungu. Nyama ya kuku hawa haina virutubisho sawa na kuku wa kienyeji.
Hii inatokana na ukweli kwamba kuku wa kizungu hulishwa madawa mbalimbali ya kuwakinga na magonjwa na hulishwa vyakula vilivyochanganywa madawa ili wakue upesi.
Kwa mazingira hayo, nyama itokanayo na kuku wa aina hii haiwezi kuwa bora.
Kiasili kuku huishi mazingira huru kwa kula vyakula ambavyo hujenga na kuukinga mwili wake dhidi ya magonjwa mbalimbali, kuku wa aina hii ndiye anayefaa kuliwa na kuleta faida ya nyama ya kuku inayokusudiwa.
MAYAI
Halikadhalika, mayai yanayopatikana kwa wingi mijini ni yale yatokanayo na kuku wa kufuga. Kiasili, mayai ya kuku wa kufuga, hayawezi kuwa sawa na mayai yatokanayo na kuku wa kienyeji. Huhitaji kuwa mwanasayansi kuona tofauti kati ya yai la kuku wa kienyeji na kuku wa kufuga, kwani mayai hayo yakipikwa huwa tofauti kwa ladha na hata rangi.
Ni ukweli ulio wazi kuwa kuku wa kufugwa hulishwa vyakula vya kutengeneza ambavyo ndani yake huwekwa kemikali na madawa mbalimbali, wakati kuku wa kienyeji hula vyakula asili kwa kujitafutia wenyewe na mazingira wanayoishi ndiyo yanayowafanya wawe tofauti na bora. Hivyo ni dhahiri kwamba mayai tunayokula ya kuku wa kizungu yana madhara zaidi kuliko faida mwilini.
SODA
Moja ya vinywaji vinavyopendwa na kutumiwa na watu wengi ni pamoja na soda. Matangazo mengi ya biashara yanafanyika kutangaza kinywaji cha soda na kuonesha kuwa ni kinywaji ambacho hakina madhara kabisa kwa mtumiaji. Kwa matangazo hayo na kampeni hizo, familia nyingi zimeamini kuwa soda ni kinywaji bora na hata watoto wetu wamerithishwa imani hii.
Lakini kwa upande wa pili wa kinywaji hiki, siyo kinywaji salama kama ambavyo imekuwa ikielezwa. Siwezi kusema moja kwa moja kuwa mtu huruhusiwi kabisa kunywa soda kama vile ni sumu, lakini watu walitakiwa kuelimishwa na kuelezwa madhara ya kupenda kunywa soda na athari anazoweza kuzipata mtu kiafya.
Naamini tahadhari inayotolewa kwa wanywa pombe, hata kwa wanywa soda ilipaswa kutolewa pia.
Utafiti unaonesha kuwa soda, pamoja na vikorombwezo vingine, huwekwa sukari nyingi kiasi kisichopungua vijiko sita katika chupa moja.
Kiwango hicho cha sukari ni kingi zaidi ya mara tano ya kile kinachoruhusiwa kwa mtu kutumia kwa siku. Na madhara ya sukari mwilini ni mengi, yakiwemo ya kudhoofisha kinga ya mwili na viungo kwenye sehemu za maungio na pia huongeza uzito wa mwili.
Ukitaka kujua soda ina madhara kiafya, fanya utafiti binafsi na utagundua haya ninayoyaandika.
Kunywa soda zisizopungua tatu kwa muda mfupi, kisha lala usiku kama kawaida halafu wakati wa kuamka asubuhi, usikilize mwili wako.Utaamka ukiwa na maumivu mwili mzima, utajihisi uchovu, hasa sehemu za maungio, mfano wa mtu aliyefanya mazoezi mazito au kazi nzito siku iliyopita. Hiyo ni kutokana na kuingiza kiwango kingi cha sukari mwilini.
JUISI
Katika hali ya kawaida, juisi ni kinywaji baridi kisicho na kilevi wala madhara kwa mnywaji. Lakini utakuwa sahihi ukizungumzia juisi zilizotengenezwa kwa matunda halisi bila kuongezewa vitu vingine. Katika zama hizi, hali iko tofauti, juisi nyingi tunazodhani ni vinywaji baridi visivyo na madhara kwa afya zetu na za watoto wetu, hali haiko hivyo.
Juisi nyingi zinazouzwa kila sehemu ni feki. Ni jambo lakusikitisha kuona jinsi binadamu anavyojaribu kushindana na Mungu kwa kutengeneza vitu vinavyofanana na vile alivyoumba Mwenyezi Mungu kwa ajili yetu. Juisi nyingi hutengenezwa kwa kuchanganya maji, sukari na rangi zilizotengenezwa kwa kemikali mbalimbali zikiwemo zenye ladha ya matunda.
Juisi za aina hii ndiyo nyingi na zinapatikana kila kona ya nchi hii, waathirika zaidi wakiwa watoto wetu ambao hupenda kunywa kwa kufuata utamu wa sukari nyingi zilizowekwa na ladha za matunda.
Utafiti umeonesha kemikali (Additives) zinazowekwa kwenye vinywaji hivi, hudhoofisha kinga ya mwili na huwa chanzo cha magonjwa ya saratani na mengine hatarishi. Nakusihi kuacha kunywa kabisa juisi hizo na usimpe mwanao, unamuua.
Ukiacha hizo juisi zinazotengenezwa kwa kutumia kemikali ‘mwanzo mwisho’, kuna juisi zingine zinazodaiwa kutengezwa kutokana na matunda, zipo za ‘machungwa’, nanasi’, ‘pasheni’, n.k. Yapo makampuni pia yanayojitapa kutengeneza juisi zao asilimia 100 kutokana na matunda na kwamba hakuna kinachoongezwa kingine. (100% fruit, No sugar added au No additives, huandika hivyo kwenye maboksi yao au makopo wanayoweka juisi.
Hata hivyo, utafiti wa hivi karibuni umeonesha kuwa makampuni mengi yanadanganya walaji.
Kwa sababu siyo kweli kwamba hawaongezi kitu kingine katika utengenezaji wa juisi zao za matunda. Imejulikana kuwa huweka vitu vya kufanya juisi ya kwenye boksi au chupa ikae kwa muda mrefu bila kuharibika, halikadhalika huweka vitu vya kuifanya juisi hiyo kuwa na ladha moja.
Acha nikupe mfano. Katika hali ya kawaida, ukichuma machungwa matano ya mti mmoja, lazima yatakuwa na ladha tofauti, yote hayawezi kuwa na ladha sawa japo yote yanatoka mti mmoja.
Kwa maana hiyo, kama ukitengeneza juisi kwa kutumia machungwa yaliyochumwa kutoka miti tofauti, ladha ya juisi lazima itatofautina. Lakini utashangaa kuona ladha ya jusi za maboksi zote zinafanana.
Wanachofanya ni kuweka ladha moja kwenye utengenezaji wa juisi zao kabla ya kupeleka kwa mlaji. Halikadhalika, juisi ukishaitengeneza, haiwezi kukaa kwa muda mrefu bila kuharibika.
Kwa hiyo, ili kuifanya juisi hiyo iweze kukaa kwa muda mrefu bila kuharibika, lazima iwekewe kemikali ya kuihifadhi isiharibike.Kwa kuongezewa vitu hivyo, hata kama
Kwa maelezo hayo, hatushauriwi sana kunywa juisi hizo ‘ready made’ kwa sababu zimekosa uhalisia, kwani zina madhara kwa afya zetu, licha ya maelezo na matangazo mazuri tunayopewa na watengenezaji.
Badala yake tutengeneza juisi majumbani mwetu wenyewe kwa kutumia matunda halisi ili kupata faida katika miili yetu.
Jiepushe na matumizi ya sukari nyingi katika juisi unayoitengeneza mwenyewe, kwani kwa kufanya hivyo utakuwa unaiharibu, weka sukari kidogo sana ikiwezekana acha kabisa.