Uchunguzi wa kimahakama umefunguliwa nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (RDC) dhidi ya Fils Mukoko, mwanachama wa chama tawala (UDPS), baada ya kutoa maneno ya vitisho dhidi ya raia wa nchi za Magharibi wanaoishi jijini Kinshasa.
Nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), uchunguzi umeanzishwa baada ya video kusambaa kwenye mitandao ya kijamii. Video hiyo inamuonyesha Fils Mukoko, mwanachama wa chama tawala (UDPS) na mkurugenzi mkuu wa Mamlaka ya Usafi wa Mazingira ya Kinshasa, akiwatishia raia wa nchi za Magharibi huko Kinshasa. Matamshi haya yamelaaniwa vikali na viongozi wa kisiasa huko Kinshasa.Video iliyosambaa sana kwenye mitandao ya kijamii ilimwonyesha Fils Mukoko akitishia kugawa silaha kwa vijana ili kuwashambulia raia wa nchi za Magharibi. Hatua hii ilifuatia upekuzi uliofanywa hivi karibuni nchini Ubelgiji kwenye makazi ya watu wa karibu na familia ya rais wa DRC Felix Tshisekedi.
Waziri wa Sheria aliamuru Mwendesha Mashtaka Mkuu kufungua uchunguzi mara moja ili hatua kali za kisheria zichukuliwe.
Kufuatia kashfa hiyo, Gavana wa jiji la Kinshasa alimfuta kazi Fils Mukoko, ambaye alikuwa Naibu Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Usafishaji wa Jiji la Kinshasa (RASKIN).
Msemaji wa serikali, Patrick Muyaya, alilaani vikali maneno hayo akisema ni "ya kutisha kabisa" na hayawakilishi msimamo wa serikali wala taasisi yoyote ya nchi. Pia, chama tawala cha UDPS kimejitenga kabisa na matamshi hayo.











