Thursday 31 March 2016

SERIKALI KUNUNUA NDEGE MBILI, MELI….

Serikali imepanga kununua ndege mbili mpya na meli moja kwa ajili ya Ziwa Victoria katika siku chache zijazo, imefahamika.

Mpango wa kununua ndege ulitangazwa jana na Waziri wa Uchukuzi, Profesa Makame Mbarawa alipozungumza na wanahabari Dar es Salaam wakati ule wa meli ulielezwa na Rais John Magufuli alipozungumza na wananchi waliompokea Mwanza akielekea nyumbani kwake Chato kwa mapumziko.
Rais Magufuli aliahidi kuwa Serikali itanunua meli mpya katika mwaka ujao wa fedha na kuzima kilio cha muda mrefu cha wakazi wa Kanda ya Ziwa.
Rais Magufuli alisema Serikali pia itatenga bajeti kwa ajili ya kupanua Uwanja wa Ndege wa Mwanza kufikia viwango vya Kimataifa.
Rais pia aliamuru kufunguliwa mara moja kwa Barabara ya Kayenze-Igombe iliyokuwa imefungwa kwa zaidi ya miaka miwili kwa madai ya kupisha upanuzi wa Uwanja wa Ndege wa Mwanza.
Amri hiyo ya kufungua barabara ilitekelezwa mara moja na Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, John Mongella kwa kukata kamba na kuondoa vizuizi vilivyokuwa vimewekwa kuzuia magari na wananchi, hali iliyopokewa kwa shangwe na wananchi. Akizungumzia ununuzi wa meli mpya, Rais alisema Serikali inatambua adha ya usafiri wa majini kati ya Mwanza na Kagera, hivyo atahakikisha anatimiza ahadi yake ya kununua meli hiyo katika bajeti ijayo na kuwaomba wananchi kuwa watulivu.
Kuhusu ndege Profesa Mbarawa alisema Serikali ipo mbioni kukamilisha ununuzi wa ndege mbili aina ya Bombardier Q400 kwa ajili ya Shirika la Ndege la Tanzania (ATCL) ili kufufua safari za ndani za shirika hilo.

Aliwaambia wanahabari katika hafla ya utiliaji saini ushirikiano wa mawasiliano ya anga baina ya Tanzania na Kuwait kuwa ndege hizo zitakuwa mpya kutoka katika kampuni ya Bombadier ya Canada.

0 comments:

Post a Comment