Mafuta ya kupikia yanatokana
na muunganiko wa kemikali zinazozalishwa na malighafi za asili kama vile seli
za mbegu, matunda ya mimea au wanyama.
Mafuta ni moja ya vinogesho vya chakula vinavyoongeza hamu ya kula
hasa yanapotumika kwa kukaanga vitu mbalimbali kama chapati, maandazi, chipsi,
mayai, mihogo, vitumbua, kalimati na nyama.
Mafuta pia hunogesha vyakula
mbalimbali kwa kuviongezea utamu. Baadhi ya sifa za mafuta ni kutoyeyuka katika
maji, uwezo wa kuwaka, kuzalisha nishati, kulainisha ngozi au mitambo pamoja na
uwezo wa kutibu baadhi ya maradhi na kutumika kama chakula cha binadamu au
wanyama.
Kwa miaka mingi wataalamu wa afya na
lishe, wanashauri watu kuhusu athari za ulaji wa kiasi kikubwa cha mafuta.
Ubaya wa mafuta
Ulaji wa mafuta hasa yale
yanayotokana na wanyama, yanahusishwa na matatizo mengi ya kiafya kama vile
magonjwa ya moyo, kiharusi, saratani na magonjwa ya mishipa ya damu. Kutokana
na sababu hiyo, ulaji wa mafuta mengi umekuwa ukihusishwa na kutokea kwa vifo
vya watu wengi duniani.
Katika utafiti mmoja uliochapishwa
mapema mwaka huu kwenye jarida liitwalo The Journalof the American Heart Association, watafiti waligundua kuwa watu wengi wanapata
magonjwa ya moyo kutokana na kula kiasi kikubwa cha mafuta yatokanayo na mazao
ya wanyama.
Pia utafiti huo ulibaini kuwa
takribani watu 700,000 sawa na asilimia 10 ya wale wanaokufa kutokana na
magonjwa ya moyo duniani kote, chanzo ni kula kiasi kikubwa cha mafuta mabaya
kuliko yale mazuri ambayo ni muhimu katika kuimarisha afya.
Dk Dariush Mozaffarian mmoja wa
watafiti hao wa Chuo cha Sera na Sayansi ya Lishe cha Tufts Friedman nchini
Marekani anasema, Dk Dariush Mozaffarian, mmoja wa watafiti hao wa Chuo cha
Sera na Sayansi ya Lishe cha Tufts Friedman nchini Marekani, anasema ingawa
wataalamu wengi wamekuwa wakisisitiza zaidi kupunguza ulaji wa mafuta
yatokanayo na wanyama, ipo haja ya kuwapunguzia watu hofu dhidi ya aina zote za
mafuta ya kula.
Ni vizuri watu wakaelezwa umuhimu wa
kutumia kiasi cha kutosha cha mafuta mazuri yanayoimarisha afya.
Baadhi ya faida za mafuta ya kula
katika mwili wa binadamu ni pamoja na kufanya kazi kama chanzo cha nguvu na
nishati, kusaidia mwili ili uweze kusharabu vitamini A, D, E na K kutoka katika
utumbo na kuzisafirisha sehemu mbalimbali za mwili kwa ajili ya kulinda afya ya
mwili.
Vitamini hizi ni muhimu kwa ajili ya
afya ya mifupa, mishipa ya fahamu, utendaji mzuri wa seli za kinga ya mwili na
uzalishaji wa insulini inayorekebisha kiwango cha sukari mwilini.
Kiasi cha wastani cha mafuta mazuri
pia kinasaidia mwili kuzalisha lehemu nzuri ambayo ni muhimu kwa ajili ya
kutengeneza vichocheo vya homoni, kuzalisha nyongo, afya nzuri ya kuta za
utumbo, utendaji mzuri wa ubongo, kupunguza msongo wa mawazo na ukuaji mzuri wa
mwili.
Aina za mafuta
Kimsingi mafuta yanatokana na
kemikali zinazojulikana kama triglycerides ambazo zinaundwa na molekuli za
glycerin au glycerol pamoja na tindikali.
Mafuta ya kula yamegawanyika katika
makundi makuu mawili,kuna mafuta dabwadabwa; yaani mazito yanayoganda na yale
yaliyoko katika hali ya kimiminika wakati wote; yaani yasiyoganda katika joto
la kawaida la ndani ya nyumba.
Mafuta dabwadabwa yana kiasi kikubwa
cha lehemu na kwa sababu hiyo, huchochea ini lizalishe kiasi kikubwa cha lehemu
mbaya.
Mafuta yasiyoganda (yaliyo katika hali ya kimiminika wakati wote),
yana kiasi kidogo cha lehemu na kwa sababu hiyo, yanapunguza kiasi cha lehemu
mbaya na kuongeza nzuri ndani ya damu.
Kwa sehemu kubwa mafuta dabwadabwa au
mafuta mazito yanatokana na mazao ya wanyama kama vile nyama yenye mafuta,
maziwa, siagi, jibini na mayai.
Kwa mfano, maziwa ya ng’ombe yana
asilimia 65.8 ya mafuta mazito, maziwa ya mbuzi yana asilimia 66.4 ya mafuta
mazito na maziwa ya binadamu yana asilimia 48.1 ya mafuta mazito na asilimia
51.9 ya mafuta mazuri kwa afya. Hii ni kwa mujibu wa Dk George Pamplona-Roger
katika kitabu chake kiitwacho The Ecyclopedia of Foods and Their Healing Power.
Lehemu mbaya inapatikana kwenye
mafuta ya nyama nyekundu, ngozi ya nyama nyeupe kama vile ya kuku na mayai hasa
yaliyokaangwa au kiini cha yai lililochemshwa.
Wakati wataalamu wa afya
wanapendekeza kuwa ulaji wa lehemu kwa siku usizidi miligramu 300 au miligramu
200 kwa watu walioko kwenye hatari ya kupata magonjwa ya moyo, yai moja
linakadiriwa kuwa na kiasi cha miligramu 200.
Mafuta dabwadabwa pia yanaweza
kuzalishwa na mazao ya mimea kama mafuta ya nazi. Ingawa mafuta ya nazi ni
mazito, wanasayansi kwa mujibu wa utafiti uliochapishwa mwaka 2009 nchini
Brazil katika jarida la Lipids, wanadai kuwa ni mazuri kwa afya kwa vile
tindikali za mafuta katika molekuli zake haziongezi kiasi kikubwa cha lehemu
mwilini. Baadhi ya watafiti wanadai kuwa ni mazuri kwa afya ya ubongo na tezi
shingo.
Matumizi makubwa ya mafuta dabwadabwa
yanasababisha mwili kunenepa kupita kiasi, kwa vile yanakwenda kujikusanya
katika misuli, chini ya ngozi na kujishikiza kwenye kuta za mishipa ya damu.
Kwa sababu hiyo, mafuta haya yanaweza kuwa chanzo cha magonjwa ya moyo,
kiharusi na magonjwa ya mishipa ya damu.
Kwa upande mwingine, mafuta
yasiyoganda yanatambulika kuwa ni mazuri kwa afya. Yanaimarisha afya ya mishipa
ya damu, moyo na kupunguza kiasi cha lehemu mbaya mwilini. Mafuta haya pia
yanasaidia mwili kurekebisha kiasi cha sukari katika damu na tezi shingo
kufanya kazi vizuri.
Mafuta haya kwa sehemu kubwa
yanatokana na mazao ya mimea kama vile mbegu, kokwa na matunda. Lakini pia
mafuta yasiyoganda yanaweza kuzalishwa na mazao ya wanyama kama vile samaki.
Mafuta ya samaki yanadaiwa kuwa ni
bora zaidi kwa afya ya moyo na ubongo kutokana na kiasi cha kutosha cha yale
mazuri ya omega 3.
Mafuta haya pia yanaimarisha afya ya
utumbo, yanazuia na kutibu tatizo la baridi yabisi au jongo pamoja na kupunguza
uwezekano wa kupata magonjwa ya mwili yanayotokana na mzio kama vile pumu na
magonjwa ya mzio wa ngozi. Mafuta haya pia yanapunguza uwezekano wa mtu kupata
maradhi ya kipanda uso na wasichana kusumbuliwa na matatizo ya tumbo kuuma
wakati wa hedhi.
Mafuta yasiyoganda yanayotokana na
nafaka, kokwa na mbegu za mimea na yanaweza kuchakatwa viwandani na
kubadilishwa kuwa dabwadabwa yaani mazito.
Mafuta haya yakichemshwa kwa joto
kali linalofikia nyuzi 200 za jotoridi na kuongezewa haidrojeni, baadhi ya
tindikali takribani asilimia 15, hubadilika na kuwa dabwadabwa kiasi kwamba
yanaganda katika hali ya joto la kawaida la ndani ya nyumba.
Hapo ndipo mafuta haya yanakuwa ni
mabaya kwa sababu huweza kujirundika ndani ya mishipa ya damu na matokeo yake
kufanya njia kuwa ndogo.
Hali hiyo, husababisha moyo kutumia
nguvu nyingi kusukuma damu na kusababisha shinikizo kubwa la damu. Hali hiyo
ikiendelea huwa rahisi kusababisha magonjwa sugu kama vile kiharusi na
kisukari. Pia mafuta yanayojirundika kwenye tishu na nje ya ogani mbalimbali
mwilini husababisha uzito kupita kiasi na unene uliokithiri.
Mafuta mazito ambayo watu wengi
hupendelea kuyatumia kwa kupaka kwenye mkate, yanaweza kuchochea uzalishaji wa
kiasi kikubwa cha lehemu mwilini.
Kwa ajili ya afya bora, jamii
inashauriwa kuepuka matumizi ya mafuta yanayoganda na hata kuepuka kula nyama
yenye mafuta mengi. Ni vizuri kuongeza utumiaji wa mafuta yasiyoganda hasa yale
yanayotokana na samaki pamoja na mimea.
Ni vizuri pia kufanya mazoezi na kazi
nzito kila siku ili kupunguza kiasi cha mafuta yanayorundikana katika misuli,
chini ya ngozi na katika mishipa ya damu.
Kwa kuzingatia haya, jamii itapunguza
mzigo wa magonjwa sugu yasiyoambukiza ambayo yanaathiri ubora wa afya na uchumi
wa familia pamoja na taifa kwa ujumla.
0 comments:
Post a Comment