Wednesday 2 March 2016

AJIKATA UTUMBO KWA KUNYIMWA CHAKULA..!!

Kijana mwenye umri wa miaka 30 amefanya tukio la kushangaza, kwa kujipasua tumbo kwa wembe na kuukatakata vipande utumbo wake.

Mkazi huyo wa Kijiji cha Kinonko Wilaya ya Kakonko Kigoma Furaha John, alifikia uamuzi huo Februari 28, baada ya jaribio la kujinyonga kwa kutumia kamba kushindikana.
John ambaye anaelezwa kuwa ni mfanyabiashara wa pombe za kienyeji, aliamua kujiua kutokana na hasira za kudhulumiwa Sh35,000 na pia kunyimwa chakula na mkewe.
Akisimulia mkasa huo John ambaye amelazwa katika Hospitali ya Wilaya ya Kibondo, amesema alirejea nyumbani akiwa na hasira za ‘kurushwa’ fedha zake na mfanyabiashara mwenzake.
Amesema nyumbani nako alikutana na tukio la kunyimwa chakula na mkewe, jambo lililomuongezea hasira na kuona bora afe.
Mashuhuda wa tukio hilo walisema John alifikishwa hospitali pamoja na vipande viwili vya utumbo alivyovikata, lakini madaktari walivitupa baada ya kuharibika kwa kukaa nje ya tumbo kwa muda mrefu.
Baba mzazi wa kijana huyo Juma Nkonkoili, amesema kitendo hicho kimeisikitisha familia kwa sababu si jambo la kawaida mtu kujitoa utumbo na kuanza kuukatakata mwenyewe, kwa lengo la kujiua.

Kaimu mganga mfawidhi wa hospitali hiyo Dk Adam Jonathan, amesema madaktari walifanikiwa kuokoa maisha ya mgonjwa huyo baada ya kumfanyia upasuaji kurekebisha utumbo wake.

0 comments:

Post a Comment