Nchini Marekani
kila baada ya dakika 10 mtu mmoja huwekwa kwenye foleni ya watu wanaosubiri
kuwekewa moyo mpya ili kuweza kuendelea kuishi.
Hali hii hutokea
baada ya moyo wa mgonjwa kuonekana hauwezi kufanyiwa matibabu na hivyo njia
pekee ya kuokoa maisha yake ni kupata moyo mpya ambao huwekewa kwa njia ya
upasuaji (transplant).
Shirika la Umoja
wa Kuchangia Viungo, linasema kuwa takribani watu 22 hufariki dunia kila siku
nchini Marekani wakiwa katika foleni ya kusubiri mtu wa kujitolea moyo kwa
ajili ya kuokoa maisha yao.
Hata hivyo
wagonjwa wa aina hii sasa wanaweza kufurahia baada ya ugunduzi wa moyo wa
bandia, ambao inawezekana wakautumia kwa maisha yao yote (Total Artificial
Heart) TAH).
Mtu anayechangia
moyo (donor) anaweza kuwa ni mtu ambaye tayari ubongo wake umekufa lakini mwili
bado una uhai na hivyo moyo wake kuwa mzima, mgonjwa wa aina hii hawezi kupona.
Mgonjwa yeyote
ambaye ana hali mbaya lakini ugonjwa wake hauhusiani na moyo na ambaye hawezi
kupona pia anaweza kujitolea moyo.
Mtu aliyefariki
pia anaweza kutolewa moyo na kusaidia wenye uhitaji lakini mara nyingi hii huwa
ni kwa ridhaa yake kabla hajafariki.
Ukiwa
umegunduliwa kwa mara ya kwanza takribani miaka 60 iliyopita, moyo wa bandia wa
wakati huo uliwawezesha wagonjwa waliokuwa wakisubiri kupata mtu atakayejitolea
kupatikana na uliweza kumsaidia mgonjwa kwa muda tu.
Ugunduzi huu
mpya, unaweza kutoa suluhisho la kudumu kwa kuwa moyo huo unalenga kumwezesha
mgonjwa kuishi maisha yake yote.
Historia
inaonyesha kuwa, kipindi kirefu ambacho mgonjwa ameweza kuishi kwa msaada wa
teknalojia ya moyo wa bandia, uliojulikana kitaalamu SynCardia temporary TAH ni
miaka minne.
Katika kile
ambacho kinaelezwa kama hatua nzuri ya ugunduzi, Kampuni inayohusika na
matatizo ya moyo ya nchini Marekani inayojulikana kama SynCardia Systems Inc
inaendesha utafiti na kufanya uchambuzi wa kina kuona kama TAH inaweza kuwa
suluhisho la kudumu kwa wagonjwa wanaohitaji kubadilishiwa moyo na kushindwa
kuupata kwa wakati kutokana na kuongezeka kwa mahitaji.
“Mwishoni mwa
miaka ya 1960 wakati wagonjwa walipoanza kuwekewa mioyo mipya kutoka kwa
binadamu wengine, upatikanaji wa kiungo hicho muhimu kwa maisha ya binadamu
ulikuwa mkubwa. Upatikanaji wake ulikuwa mkubwa kuliko mahitaji lakini kwa sasa
mahitaji yameongezeka zaidi na upatikanaji umepungua,” anasema Danald Isaacs
ambaye ni Makamu wa Rais wa SynCardia, akiliambia Shirika la Habari la Fox.com.
Idara ya Afya na
Huduma za Binadamu ya Marekani inakadiria kuwa watu 4,000 husubiria kupata moyo
mpya ili waweze kuendelea kuishi kila siku wakati mioyo 2,300 ikiwa inatolewa.
Ugonjwa wa moyo
ni chanzo namba moja cha vifo nchini Marekani ukigharimu maisha ya watu 611,000
mwaka 2015, hii ni kwa mujibu wa Kitua cha Kupambana na Kuzuia Magonjwa cha
nchi hiyo (CDC)
Wakati wa
kumwekea mgonjwa moyo wa bandia au TAH, daktari huondoa kwa njia ya upasuaji
ventrikali ya kulia pamoja na valvu nne kama ambavyo hufanyika wakati mgonjwa
akiwekewa moyo ambao hutolewa na binadamu mwingine ambapo huwekwa wa bandia
badala yake.
“Asilimia 96 ya
mfumo wa kuweka moyo bandia ni ule wa SynCardia Temporary TAH ambao hutoa
suluhisho la muda tu,” anasema Isaacs. Takwimu za
SynCardia zinaonyesha kuwa wagonjwa 1,123 wamewekewa mfumo huo ambao ni modeli
70cc.
John Beckingham,
mwenye umri wa miaka 58 ambaye ni mhandisi mstaafu anayeishi katika eneo la
Rochester jijini New York alifanyiwa upasuaji uliofanikisha kuwekewa moyo mpya
katika hospitali ya Cleverland, Oktoba mwaka 2015 baada ya kukaa miezi sita
kwenye foleni ya kusubiria. Wakati akisubiria alikuwa akitumia mashine maalumu
ambayo ilikuwa ikitumia betri na ambayo ufanisi wake haukuwa sawa na
teknalojia hii mpya.
0 comments:
Post a Comment