Friday, 3 February 2017

KIKONGWE MIAKA 75 AJIUNGA DARASA KWANZA..

Nyamohanga Suguta (75) mkazi wa Kitongoji cha Kibeyo Kijiji cha Getenga Kata ya Mbogi wilayani Tarime, amejiunga na darasa la kwanza mwaka huu katika shule mpya ya msingi ya Makerero baada ya kuamua kusoma.

Mwalimu Mkuu wa Shule hiyo Riziki Focus, amesema mwanafunzi huyo amejiunga na darasa la kwanza kutokana na kufanya vizuri katika darasa la utayari kwa masomo yake ya kazi za mikono, hesabu na mwandiko.
Akizungumza katika uzinduzi wa shule hiyo juzi Focus amesema kuwa, mwanafunzi huyo aliandikishwa darasa hilo mwaka huu katika Mpango wa Elimu ya Msingi kwa Watoto Walioikosa (Memkwa).
Shule ya Msingi Makerero ilifunguliwa Februari mosi mwaka huu na Kaimu Ofisa Elimu Msingi Tumaini Musoma, kwa niaba ya Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Tarime Apoo Tindwa.
Hivi sasa ina wanafunzi 66 wa darasa la kwanza akiwamo Suguta wakati wa awali wakiwa   46.
Akielezea uamuzi wake wa kujiunga na shule, Suguta amesema ameamua kufanya hivyo baada ya kuvutiwa na elimu.

Suguta amesema aliwahi kusoma na kukomea darasa la pili mwaka 1950, kutokana na kukumbwa na mazingira magumu na kulazimishwa kuchunga mifugo na kulima na familia yake.

Reactions:

0 comments:

Post a Comment