Thursday, 16 February 2017

ALIYETEULIWA NA TRUMP KUWA WAZIRI AJITOA..

Andrew Puzder aliyekuwa ameteuliwa na Rais wa Marekani Donald Trump kuwa waziri wa masuala ya wafanyakazi, amejiondoa muda mfupi kabla ya kuhojiwa na wabunge.

Puzder alipoteza uungwaji mkono wa maseneta kadha wa chama cha Republican baada yake kukiri kwamba alimwajiri mhamiaji aliyeingia Marekani kinyume cha sheria kuwa mjakazi.
Bilionea huyo pia amekosolewa kwa matamshi yake kuhusu wanawake na wafanyakazi katika migahawa yake.
Yeye sasa anakuwa mtu wa kwanza miongoni mwa waliopendekezwa na Trump kuwa waziri kukosa kuidhinishwa.
Talaka yake na mkewe mwaka 1980 ambayo ilikumbwa na mvutano mkubwa, pia imemwathiri.
Majuzi ilibainika kwamba mke wake wa zamani Lisa Fierstein, alishiriki kama mwathiriwa wa udhalilishaji kwenye ndoa, katika kipindi cha Oprah Winfrey mwaka 1990 ambacho kilifahamika kwa jina High Class Battered Women (Wanawake wa tabaka la juu wanaopigwa na waume zao).
Walitalikiana mwaka 1987 lakini baadaye aliondoa tuhuma za udhalilishaji dhidi ya Puzder, wakati wa makubaliano kuhusu nani angewatunza watoto.

0 comments:

Post a Comment