Wednesday 15 February 2017

MAKAMANDA WA MIKOA WATAKIWA KUONGEZA NGUVU VITA DHIDI YA DAWA ZA KULEVYA…

Katika kuhakikisha kuwa biashara haramu ya dawa za kulevya inakomeshwa hapa nchini na kwa kuzingatia dhamira ya serikali ya awamu ya tano ya kupambana na tatizo la dawa
za kulevya, jeshi la polisi nchini limetoa maelekezo kwa Makamanda wa Polisi katika mikoa yote kuongeza nguvu za Oparesheni dhidi ya biashara hiyo haramu kwa kuwakamata wanaotumia, wanaouza na wanaosafirisha.
Jeshi hilo limewaagiza Makamanda wote pindi wanapoendesha oparesheni dhidi ya dawa za kulevya kutokuangalia sura ya mtu, cheo, wadhifa wala nafasi aliyonayo katika jamii.
Katika hatua nyingine, Jeshi la Polisi nchini linakemea vikali tabia ya baadhi ya wananchi wanaokusanyika katika vituo vya Polisi pindi baadhi ya watuhumiwa wa makosa mbalimbali wanapotakiwa kufika kwenye vituo hivyo kwa ajili ya kuhojiwa kuhusiana na tuhuma wanazokabiliwa nazo.
Limesema ni marufuku kwa mtu ama kikundi chochote kukusanyika katika kituo cha Polisi bila ya kuwa na sababu ya msingi na watakaobainika watashughulikiwa kwa mujibu wa sheria.
Jeshi la Polisi nchini, linatoa wito kwa wananchi kuendelea kutoa taarifa za uhalifu na wahalifu zikiwemo za watu wanaojihusisha na biashara haramu ya dawa za kulevya na taarifa hizo zitafanyiwa kazi kwa siri ili kuhakikisha nchi inaendelea kuwa katika hali ya usalama.
Imetolewa na:
Advera John Bulimba-ACP,
Msemaji wa Jeshi la Polisi,
MAKAO MAKUU YA POLISI.

0 comments:

Post a Comment