Mvutano umeibuka
bungeni kati ya Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani, Freeman Mbowe na Naibu
Spika, Dk Tulia Ackson baada ya Mbunge huyo wa Hai kumwuliza Waziri Mkuu,
Kassim Majaliwa swali lililopingwa na Naibu Spika kwa maelezo kuwa ni la
kisheria si la kisera.
Sakata hilo liliibuka
asubuhi katika kipindi cha maswali kwa Waziri Mkuu, baada ya Mbowe kuhoji
sababu za Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema kusota rumande kwa kukosa
dhamana, Peter Lijualikali wa Kilombero anayetumikia kifungo cha miezi sita gerezani
na wanachama wengine wa Chadema wanaokabiliwa na mashitaka mbalimbali.
Mbowe alimtaka
kiongozi huyo wa shughuli za Serikali bungeni, aeleze kama ni sera ya Serikali
kuua vyama vya upinzani, huku akisema Rais John Magufuli alipata kutamka kuwa
atavimaliza vyama vya upinzani kabla ya mwaka 2020.
Kwa maswali hayo, Dk
Tulia alimtaka Waziri Mkuu kujibu swali linalohusu sera na kuachana na
yanayogusa masuala ya kisheria.
Jambo hilo liliwafanya
wabunge wa Upinzani huku wakipiga meza kwa takribani dakika tano kupinga,
wakimtaka Naibu Spika aache Waziri Mkuu ajibu swali hilo.
Katika swali lake la
msingi, Mbowe alisema wakati jana ikiwa ni Siku ya Haki Duniani, imepita miezi
mitatu tangu Lema aanze kusota rumande huku akinyimwa dhamana licha ya kuwa iko
wazi.
Pia alisema
Lijualikali anatumikia kifungo cha miezi sita jela kwa kosa la kisiasa sambamba
na mwenyekiti wa chama hicho wa mkoa wa Lindi, Suleiman Mathew aliyefungwa miezi
minane na madiwani zaidi ya sita na viongozi wengine 215 nao wakifungwa au
kuendelea na mashitaka huku zikifanyika hila za kuidhoofisha CUF.
“Haya yanayoendelea
katika Serikali ambayo ni kinyume na utamaduni na mazoea yetu kama Taifa, je ni
utekelezaji wa sera ya kuua upinzani chini ya Rais Magufuli?” Alihoji Mbowe.
Kabla ya Waziri Mkuu
kujibu swali hilo, Dk Tulia aliingilia kati na hali kuwa hivi:
Dk Tulia: Katika swali lako kuna masuala ya kisera
na kisheria. Maswali yanayomhusu Lema na Lijualikali na madiwani sita ni ya
kisheria, hayo kuhusu leo (jana) kuwa siku ya haki duniani, Waziri Mkuu anaweza
kuyajibu.
Majaliwa: Nakanusha, Rais hajawahi kutangaza kuvifuta
vyama vya upinzani, nchi inaongozwa kwa sheria, kanuni na taratibu na kuna
Bunge, Serikali na Mahakama.Hakuna mhimili unaoingilia mhimili mwingine. Jambo
lililopo mahakamani halizungumzwi kokote, siwezi kuzungumzia hilo.
Mbowe: Kwa kuwa Rais anaonekana kuvunja Katiba
ikiwa ni pamoja na kupiga marufuku mikutano ya vyama vya siasa, je tukileta
ushahidi kuwa Rais amekusudia kuumaliza upinzani kabla ya 2020, Waziri Mkuu
utakuwa tayari kuwajibika kwa kujiuzulu?
Dk Tulia: Mbowe swali lako la maelezo ya jumla,
yako sawasawa ila la kumtaka Waziri Mkuu kuwajibika si la kisera, kuwajibika si
sera uliza swali la kisera.
Mbowe: Labda swali langu nilielekeze kwa Naibu Spika
(Dk Tulia). Swali langu lilikuwa la mwendelezo ambalo hutokana na majibu ya
msingi yaliyotokea. Kama kulikuwa na msingi wa kisera kwenye swali la msingi,
swali la mwendelezo linakwenda kutokana na majibu yaliyotolewa. Waziri Mkuu
aseme tu kama yupo tayari kujiuzulu tukileta ushahidi.
Katika maelezo yake,
Dk Tulia alitaka Mbowe ajikite katika swali la kisera jambo ambalo Mwenyekiti
huyo wa Chadema alipinga na kusisitiza kuwa huenda mambo yanayofanyiwa
wapinzani, wabunge, mawaziri Serikali inayafurahia.
0 comments:
Post a Comment