Sunday 5 February 2017

WHO: Saratani ilisababisha hasara ya dola trilioni 1.6 duniani mwaka 2010

Shirika la Afya Duniani, WHO limesema gharama za matibabu ya saratani ni kubwa kuliko zile za kinga na tiba wakati wa hatua za mwanzo za ugonjwa huo unaosababisha kifo cha mtu mmoja katika kila watu sita duniani kote.

WHO imetolea mfano mwaka 2010 ambapo gharama za kiuchumi na kiafya zilizotokana na saratani ilikuwa dola trilioni 1.16 duniani kote.
Ili kupunguza gharama, WHO imezindua mwongozo mpya wa kuwezesha nchi yoyote bila kujali kipato chake iweze kuimarisha ugunduzi wa saratani mapema.
WHO ilitoa kauli hiyo Jumamosi Februari Nne ambayo ni Siku ya Saratani Duniani. Kwa munasaba wa siku hiyo WHO imezindua mwongozo mpya wa kuwezesha uchunguzi wa mapema wa ugonjwa huo hatari unaosababisha vifo vya watu milioni 8.8 kila mwaka duniani, kati ya wagonjwa milioni 14 wanaobainika kuwa nao.
WHO inasema hali si shwari kwani idadi inaongezeka mwaka hadi mwaka na hivyo njia pekee ni kuimarisha mbinu za kubaini mapema kwani hata visababishi vya saratani navyo vinaongezeka.
Shirika hilo linasema saratani haipaswi kusalia adhabu ya kifo wakati huu ambapo kuna kampeni za kudhibiti visababishi kama vile matumizi ya tumbaku, unywaji wa pombe na mlo usio bora.

0 comments:

Post a Comment