Tuesday, 14 February 2017

MAHARUSI WALIOTUMIA DOLA PEKEE WAANDALIWA HARUSI YA KIFAHARI KENYA

Maharusi waliowasisimua wengi baada ya kutumia Sh100 pekee za Kenya kugharimia harusi, wameandaliwa sherehe ya harusi ya kufana jijini Nairobi.

Sherehe hiyo ya marudio imeandaliwa katika bustani ya Eden Bliss, Nairobi ulimwengu ukiandhimisha Siku ya Wapendanao.
Harusi ya Anne na Wilson Mutura ya awali iligharimu dola moja pekee ya Kimarekani lakini sherehe ya sasa imegharimu takriban Sh3.5 milioni (Dola 35,000).
Pesa hizo zimegharimiwa na makundi mbalimbali yanayohusika katika uandaaji wa sherehe, ambayo yaliungana kwa pamoja na kuchanga pesa kuandalia Anne na Wilson sherehe ya kukata na shoka.
Wawili hao wanaoishi eneo la Kasarani Nairobi, walisifiwa kwa kuonyesha thamani halisi ya mapenzi badala ya kuongozwa na pesa.
Kando na kuandaliwa harusi hiyo, wametunukiwa shamba la kilimo cha kisasa, fungate kwenye hoteli ya kifahari na baada ya sherehe ya leo wanatarajiwa kwenda kwa fungate nyingine mjini Dubai.
Dola yenyewe walioyotumia Anne na Wilson katika harusi yao waliitumia kununua pete mbili.
Walikuwa wameahirisha harusi yao mara tatu baada ya kukosa fedha za kutosha kuandaa sherehe kubwa ya harusi.
Maombi yao kwa familia na marafiki kuwafanyia mchango, hayakutimizwa.
Baada ya muda Bwana harusi Wilson, hakuwa na la kufanya ila kumshawishi mpenzi wake kuhusu uwezo wake.


Reactions:

0 comments:

Post a Comment