Monday 13 February 2017

WAFIKA POLISI KUOMBA WAPEWE DAWA ZA KULEVYA........

Katika hali isiyokuwa ya kawaida, baadhi ya waathirika wa dawa za kulevya maarufu kwa jina la ‘mateja’ wamefika makao makuu ya polisi mkoa wa Mbeya kuomba wapewe dawa hizo kidogo kwani zimeadimika mtaani.

Waathirika hao wamedai kuwa tangu kuanza kwa kampeni ya vita dhidi ya dawa za kulevya jijini Dar es Salaam, cheche zake zimepelekea dawa hizo kuadimika mitaani na kwamba waathirika wako katika hali mbaya kwa kukosa dawa hizo, hivyo walichukua uamuzi wa kwenda polisi kuomba wapewe japo kidogo kuwanusuru.
“Tunawaomba ninyi waandishi mtusaidie, Serikali iachie kidogo dawa za kulevya. Vijana mateja waliokuwa wakitumia watakufa wote kwani vijiwe vingi kwa sasa havina dawa,” muathirika aliyefika polisi na baadae kuzungumza na mwandishi wa habari wa Mwananchi anakaririwa.
Kamanda wa Polisi mkoa wa Mbeya Dhahiri Kidavashari alithibitisha kuwa mateja hao walifika ofisini kwake wakiomba kupewa dawa kidogo za kulevya kujinusuru na ‘arosto’, lakini walihojiwa na kupelekea kukamatwa kwa wafanyabiashara wawili wakubwa wa dawa hizo ambao wanaendelea kushikiliwa kwa mahojiano zaidi.
Katika hatua nyingine, Kamanda Kidavashari alisema kuwa jeshi hilo linaendelea kumshikilia na kumhoji mwanafunzi aliyekamatwa akiuza dawa za kulevya aina ya kokeni na kwamba mama yake mzazi amekimbilia kusikojulikana
Vita hiyo dhidi ya dawa za kulevya inaendelea huku jiji la Dar es Salaam likionekana kuwa kitovu cha mapambano yanayotoa cheche kali mikoani ambapo leo Mkuu wa Mkoawa Dar es SalaamPaul Makonda anatarajia kuachia orodha ya awamu ya tatu ya watu wanaotuhumiwa kujihusisha na dawa za kulevya mkoani humo

0 comments:

Post a Comment