Thursday 2 February 2017

MAJALIWA: RAIS HAJATANGAZA KUFUTA VYAMA VYA UPINZANI

 
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amesema Rais Dkt. John Magufuli hajawahi kutangaza ama kutoa kauli ya kufutwa kwa vyama vya siasa nchini.

Ameyasema hayo leo Bungeni mjini Dodoma wakati akijibu swali la Kiongozi wa Kambi ya Upinzani Bungeni, Freeman Mbowe  katika kipindi cha maswali na majibu kwa Waziri Mkuu.
Mbowe amesema Rais Dkt. Magufuli alinukuliwa akisema atahakikisha anafuta vyama vya upinzani ifikapo mwaka 2020 ata hakikisha hakuna upinzani nchini, pia alitaka kujua nini kauli ya Serikali kuhusu kunyimwa dhamana kwa Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema ambaye anashikiliwa kwa muda miezi mitatu.
Aidha, wakati akijibu swali hilo Waziri Mkuu amesema kuwa Rais Dkt. John Magufuli hajawahi kutangaza kufutwa kwa vyama vya siasa ifikapo 2020.
“Kwanza nataka nikanushe kwamba Mheshimiwa Rais hajawahi kutangaza kuvifuta vyama vya upinzani. Pia Watanzania wote wanajua nchi hii inaongozwa kwa sheria, kanuni na taratibu,” amesema Waziri Mkuu.
Amesema kuwa wanaongoza nchi kwa kufuata mihimili mitatu ambayo ni Serikali, Mahakama na Bunge na kwamba hakuna mhimili unaoweza kuingilia mwingine.

Hata hivyo, Waziri Mkuu amewahakikishia Watanzania kwamba suala la upungufu wa sukari halitatokea nchini kwa sababu viwanda vya ndani vinaendelea kuzalisha na hadi mwishoni mwa Januari vilifikia asilimia 86 ya uzalishaji.

0 comments:

Post a Comment