Wednesday, 22 February 2017

NASA WATATANGAZA NINI KUHUSU MFUMO WA JUA?

Shirika la Anga za Juu la Marekani (Nasa) leo linatarajiwa kutangaza ugunduzi "mkubwa" kuhusu mambo yaliyomo "nje ya mfumo wetu wa jua".
Hafla ya kutangaza ugunduzi huo itapeperushwa moja kwa moja kupitia runinga ya Nasa na katika mtandao wa shirika hilo mwendo wa saa kumi na mbili jioni (GMT) ambazo ni sawa na saa tatu Afrika Mashariki Jumatano jioni.

Habari kuhusu tangazo hilo pia zitachapishwa katika jarida la kisayansi la Nature na baadaye katika Reddit AMA (Ask Me Anything/Niulize Chochote).
Je, ni baadhi ya mambo gani wataalamu Nasa wanaweza kuwa wanataka kuwatangazia watu?
Nasa watatangaza kugunduliwa kwa viumbe hai anga za juu?

Kuna uwezekano kwamba amegundua viumbe wanaoishi anga za juu?

Hili ni suala la kwanza watu kulifikiria, na tayari kunao wanaolijadili kwenye Twitter.

Lakini usisikitike sana iwapo hakutakuwa na ugunduzi wowote kama huo.

Moja ya viashiria vya kuwepo na viumbe hai anga za juu au katika sayari nyingine ni uwepo wa maji.

Mwaka 2015, Dkt Joe Michalski wa Makumbusho ya Historia ya mambo Asilia London alisema, "Duniani, popote unapopata maji, huwa kuna uhai."

Wakati huo, Nasa walikuwa wanatangaza kugunduliwa kwa kiowevu juu ya Mars. Maeneo yenye kiowevu hicho Mars yalitajwa kuwa pahala pazuri pa kutafuta viumbe walio hai, kwa hivyo huenda Nasa wamegundua maji katika sayari nyingine.

Lakini wanasayansi pia wamekiri kwamba itachukua muda kuyachunguza maji ya Mars kwa karibu na kwa kina zaidi.

Kuna makubaliano ya kimataifa ya kuzuia kufika kwa vyombo vya anga za juu maeneo ya Mars yanayodhaniwa kuwa na maji bila kutibiwa vyema, kuzuia kuingizwa kwa sumu au viumbe ambao huenda wakavuruga usafi au kuingilia yaliyopo maeneo hayo.
Nasa wamekuwa wakisema kuna uwezekano wa kuwepo maji Mars

Nasa wamesema mapema kwamba kikao hicho chao kitahusu sayari ambazo zipo nje ya mfumo wetu wa jua, kwa hivyo kuna uwezekano kubwa kwamba huenda wakawa wanazungumzia sayari kama hii.

Sayari hizo huitwa "Exoplanet" kwa Kiingereza, na huwa ni sayari ambazo zinazunguka nyota nyingine ambayo si jua.

Agosti, wanasayansi walisema nyota inayokaribia zaidi mfumo wetu wa jua ina sayasi inayokaribiana sana na dunia ambayo inaizunguka.

Waliipa jina Proxima B.

Kadhalika, sayari hiyo ambayo inazunguka nyota hiyo iliyopewa jina Proxima Centauri huzunguka katika eneo ambalo linatoa uwezekano mkubwa sana wa kupatikana kwa maji.

Lakini bado haijabainika iwapo watu wanaweza kuishi katika sayari hiyo.

Proxima inapatikana kilomita 40 trilioni kutoka kwa dunia.

Kwa kutumia teknolojia ya sasa, itachukua maelfu ya miaka kufika huko.

Kwa hivyo, kuna uwezekano mkubwa kwamba tangazo la leo linahusu Proxima B, au sayari nyingine inayokaribiana na sayari ya dunia.

Kuna pia sayari ya Pluto.

Iliacha kutambuliwa kama sayari ya tisa katika mfumo wa jua miaka 11 iliyopita.

Nasa hata hivyo wamekuwa wakipigania itambuliwe tena kuwa sayari. Wanasema imetimiza vigezo vyote vinavyohitajika kuifanya kuwa sayari. Je, watakuwa wanazungumzia Pluto?

 

0 comments:

Post a Comment