Mahakama
ya Hakimu Mkazi Arusha, imetupa pingamizi la mawakili wa Mbunge wa Arusha
Mjini, Godbless Lema la kuitaka isisikilize kesi ya kuhamasisha maandamano ya
Ukuta, bali kwanza ifikishwe Mahakama ya Katiba.
Lema, ambaye ni mbunge kupitia
Chadema, anakabiliwa na kesi hiyo akidaiwa kuhamasisha maandamano hayo ya chama
chake yaliyokuwa yamepangwa kufanyika Septemba Mosi, mwaka jana.
Mawakili wa Lema, John Mallya na
Sheck Mfinanga, waliwasilisha ombi mahakamani hapo wiki iliyopita wakitaka
kesi hiyo isikilizwe Mahakama ya Katiba kwa kuwa kuna hoja za kikatiba ambazo
zitahitaji kutolewa maelezo na majaji watatu wa Mahakama hiyo.
Katika kesi hiyo, Lema anadaiwa
kuhamasisha maandamano kwa njia ya mtandao wa kijamii (audio clip)
aliyoitengeneza na kujirekodi ujumbe mfupi wa sauti na kisha kusambaza
Agosti Mosi hadi 26, mwaka jana katika mitandao ya kijamii ya
WhatsApp.
Hakimu Bernard Nganga amesema kosa
alilofanya Lema siyo la kikatiba na hoja za kutaka kuhamishiwa shauri hilo
Mahakama ya Katiba hazina mashiko kisheria.
Amesema sheria ipo wazi, kuwa mtu
yeyote akihusika na kushawishi utendaji wa kosa hata kama halina madhara,
muhusika ana makosa na adhabu yake ni kifungo cha miaka miwili au kulipa faini.
Hakimu Nganga amesema pingamizi za
utetezi zimetupwa na shauri litaendelea kusikilizwa.
0 comments:
Post a Comment