Msanii maarufu anayepamba video za wasanii wa muziki
wa bongo Fleva (Video Queen) Agnes Gerald maarufu Masogange ameendelea kusota
rumande, huku jalada lake likiendelea kuwa mikononi mwa Mwanasheria Mkuu wa
Serikali (AG).
Masogange (25), alikamatwa na Jeshi la Polisi Kanda Maalumu ya
Dar es Salaam kwa tuhuma za kujihusisha na uuzaji, usafirisha na kutumia dawa
za kulevya.
Masogange alitarajiwa kupandishwa kizimbani Ijumaa wiki
iliyopita lakini ilishindikana kutokana na majibu ya Mkemia Mkuu wa Serikali
dhidi ya vipimo vyake kuonesha kama anatumia au hatumii dawa hizo kutokamilika.
Hata hivyo alitarajiwa kufikishwa tena Mahakama ya Hakimu Mkazi
Kisutu juzi ambapo alikwama tena kutokana na jalada lake kupelekwa kwa AG.
Wakili wa Masogange Nick Kitege alisema bado jalada la
Masogange lipo kwa AG na anaendelea kulifanyia kazi na pindi litakapokamilika
muda wowote anaweza kupelekwa mahakamani.
Alisema jalada hilo limechelewa kutokana na taratibu za kisheria
zinazofanywa ili kukamilisha uchunguzi.
Julai mwaka 2013 Masogange alikamatwa Afrika Kusini katika
Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Oliver Tambo, akiwa na mwenzake aliyejulikana
kwa jina la Melisa Edward wakiwa na mzigo wa dawa za kulevya wenye thamani ya
zaidi ya Sh bilioni 6.8.
0 comments:
Post a Comment