Tuesday, 22 March 2016

MILIPUKO YATOKEA UWANJA WA NDEGE BRUSSELS…

Moshi umeonekana ukitoka kwenye moja ya majumba katika uwanja huo
Milipuko miwili imetokea katika uwanja wa ndege wa Zaventem mjini Brussels.Moshi umeonekana ukitanda angani kutoka kwa moja ya majengo katika uwanja huo.
Serikali ya Ubelgiji imethibitisha kwamba kunao watu waliojeruhiwa lakini haijasema idadi.
Watu wameondolewa kutoka kwenye uwanja huo na safari za ndege kutua au kupaa kutoka uwanja huo kukatizwa.
Vyombo vya habari nchini humo vinaripoti kwamba kuna watu wamejeruhiwa katika ukumbi wa kuhudumia watu wa safari za kuondoka nchini na kwamba milipuko ilitokea karibu na meza ya shirika la ndege la American Airlines.
Haijabainika ni nini chanzo cha milipuko hiyo.
Milipuko pia imeripotiwa katika kituo cha treni cha Maelbeek karibu na majengo taasisi za Umoja wa Ulaya. Mfumo wa uchukuzi wa treni mjini Brussels umefungwa.
Milipuko hiyo imetokea siku nne tu baada ya kukamatwa kwa mshukiwa mkuu wa mashambulio ya Paris ya mwaka jana ambayo yalisababisha vifo vya watu 130.
Abdeslam alikamatwa Ijumaa katika mtaa mmoja wa Brussels.

Uwanja wa ndege wa Zaventem unapatikana kilomita 11 kaskazini mashariki mwa Brussels na ulihudumia abiria zaidi ya 23 milioni mwaka jana.

0 comments:

Post a Comment