Tuesday 29 March 2016

DAKTARI APIGWA NA NDUGU WA MGONJWA……

Madaktari na wauguzi wa Hospitali ya Rufani Mkoa wa Mtwara Ligula, wamegoma kutoa huduma baada ya mwenzao kudaiwa kupigwa na ndugu wa mgonjwa hadi kuvuliwa nguo.

Tukio hilo lilitokea juzi majira ya saa 5.00 asubuhi, baada ya mgonjwa kulazwa hospitalini hapo tangu Jumamosi kutokana na ajali ya pikipiki na kupewa rufaa jambo lililowaudhi.
Madaktari wa hospitali hiyo walioshuhudia tukio hilo, wamesema majeruhi alifikishwa hospitalini Jumamosi akiwa ameumia na aliendelea kupatiwa huduma.
Madaktari hao waliomba kutotajwa, wamesema mwenzao alipigwa baada ya kutoa taarifa za rufaa kwa ndugu wa mgonjwa kuwa anatakiwa kupelekwa Muhimbili.
Daktari mwingine alipoulizwa sababu za wao kutotoa huduma na kujikusanya kwenye moja ya jengo la hospitali hiyo, alidai ni kwa ajili ya usalama wao kwani kitendo alichofanyiwa mwenzao kimewafedhehesha na kuwadhalilisha.

Mmoja wa wagonjwa walioathiriwa na mgomo huo Zamda Kupwaja, amesema alifika hospitalini hapo majira ya saa 6.00 mchana, alipata cheti na alipomuona daktari alimwandikia dawa alipokwenda dukani hapakuwa na mhudumu.

0 comments:

Post a Comment