Sunday 14 April 2013

Hatari:Aina Mpya ya Kisonono Yasambaa Duniani

ina mpya ya vimelea vya ugonjwa wa kisonono au "gono" ambavyo vinahimili dawa (resistant to drugs) zinazotumika kutibu ugojwa huu imegundulika duniani. Taarifa iliyotolewa na shirika la afya duniani (WHO) hivi karibuni imesema, ugonjwa wa kisonono unaoathiri mamilioni ya watu ulimwenguni umeanza kuwa sugu dhidhi ya dawa zinazotumiwa kuutibu na hivyo kuna hatari ya kutoweza kutibika kabisa.

Shirika la afya duniani limetoa wito kwa serikali na madaktari kuongeza ufuatlijiaji wa aina hii ya kisonono kutokana na ugonjwa wa kisonono kuwa na athari nyingi kama mcharuko (inflammation), ugumba, matatizo wakati wa ujauzito na hata vifo vya kina mama wajawazito.
“Aina hii mpya ya vimelea vya kisonono vinaonyesha usugu dhidhi ya dawa zote za antibiotiki tunazotumia dhidhi yake ikiwemo dawa za jamii ya cephalosporins ambazo ni dawa za mwisho katika kutibu ugonjwa wa kisonono, “ alisema Dk. Manjula Lusti-Narasimhan, mmoja wa wanasayansi wa shirika la afya duniani katika kitengo cha magonjwa ya zinaa.
Miaka michache ijayo, aina hii mpya ya kisonono itakuwa sugu dhidhi ya dawa zote ambazo tunazo saizi “aliendelea kusema Dk. Manjula Lusti-Narasimhan wakati wa mahojiano na shirika la habari la The Associated Press kabla WHO haijatangaza rasmi hatua na mwongozo mpya wa kukabiliana na tishio la aina hii mpya ya kisonono.
Inakisiwa watu milioni 106 ulimwenguni kote huathiriwa na ugonjwa wa kisonono kila mwaka.Ugonjwa wa kisonono pia huongeza hatari ya kupata maambukizi ya ugonjwa wa Virusi vya Ukimwi (VVU).
“Ugonjwa sugu wa kisonono sio tatizo la bara la Ulaya au Afrika pekee bali ni tatizo la dunia nzima kwa sasa,’” alinukuliwa akisema Dk. Manjula Lusti-Narasimhan.
Kwa mara ya kwanza, vimelea sugu vya ugonjwa wa kisonono dhidhi ya dawa aina ya cephalosporins  viliripotiwa katika nchi ya Japan, ikifuatiwa na Uingereza, Hongkong na Norway.
Wanasayansi wanaamini matumizi mabaya ya dawa aina ya antibiotiki pamoja na uwezo wa vimelea vya ugonjwa wa kisonono kubadilika na kuzoea mazingira mapya ndio chanzo kikuu cha kutokea kwa ugonjwa sugu wa kisonono na hivyo muda si mrefu ugonjwa huu utakuwa janga kubwa dunia nzima kama hatua za haraka hazitachukuliwa. Kuna uwezekano wa vimelea hivi sugu vya kisonono vinasambaa kwa sasa duniani bila kuweza kugundulika kutokana na nchi nyingi kutokuwa na ufuatiliaji na utunzaji kumbukumbu  mzuri wa wagonjwa wake.
Shirika la afya duniani limesema nchi zinatakiwa kuongeza ufuatiliaji wa wagonjwa wake pamoja na kudhibiti matumizi holela ya dawa za antibiotiki mpaka pale taarifa kamili za ugonjwa huu zitakapojulikana.
“Elimu ya masuala ya kujamiana pamoja na matumizi sahihi ya mipira ya kondomu inahitajika ili kutokomeza kabisa ugonjwa huu sugu wa kisonono. Hatuwezi kuutokomeza kabisa ugonjwa huu bali tunaweza kuzuia usambaaji wake,”alisema Dk. Manjula Lusti-Narasimhan.

0 comments:

Post a Comment