Sunday 14 April 2013

Protini Yagundulika Kusababisha Saratani ya Matiti kwa Wanawake Wanaotumia Vilevi

Kimengenyo (enzyme) ambacho ni protini aina ya CYP2E1 kimegundulika kuwa ndio chanzo kinachochangia wanawake kupata saratani ya matiti kwa wanawake wanaotumia vilevi. Kwa muda mrefu wanasayansi walikuwa wakitafuta uthibitisho wa uhusiano wa kunywa pombe na saratani ya matiti, lakini sasa wameweza kupata uhusiano huo. Protini hii hupatikana kwenye matiti ya wanawake na hivyo kuwaweka kwenye hatari kubwa ya kupata saratani ya matiti kama watakuwa wanakunywa sana vilevi kama pombe, whiskey, wine na nk.
Utafiti uliofanywa na chuo kikuu cha Autonomous University of the State of Morelos cha nchini Mexico, umeonyesha ya kwamba protini hiyo ya aina ya CYP2E1 inauwezo wa kukivunja vunja kilewesho (ethanol) na kusababisha kutolewa kwa kemikali hatari zinazojulikana kama free radicals.
Watafiti hao wamesema ugunduzi wao utasaidia katika kuvumbua kipimo kitakachosaidia kujua ni wanawake gani walio na protini hii ya CYP2E1 na hivyo kuwasaidia kujikinga dhidhi ya saratani ya matiti.
Kemikali hizi hatari uhusishwa na kutokea kwa baadhi ya magonjwa kama saratani mbalimbali, ugonjwa wa kisukari, uharibifu wa mishipa ya damu aina ya ateri (arteries), kuchangia mtu kuzeeka na nk.
Swali kuu walilojiuliza watafiti wakati wa utafiti huo ni , Je kuwa na protini hii ya CYP2E1 kwa wingi huchangia mwanamke kupata ethanol-induced toxicity na hivyo kumhatarisha kupata saratani ya matiti?
Matokeo yetu yalionyesha ya kwamba seli za kutoka katika matiti ya mwanamke (mammary cells) zilizowekwa kilewesho cha aina ya ethanol, hutoa kemikali hatari kwa wingi, husababisha kuwepo kwa oxidative stress, huharakisha ufanyaji kazi wa seli na hivyo kuongeza kiwango cha ukuaji wa seli hizi kwa wingi na kusababisha saratani ya matiti” alisema Profesa Maria de Lourdes Rodriguez-Fragoso, kutoka chuo kikuu cha The Autonomous University of the State of Morelos cha nchini Mexico.
“Kama wewe ni mwanamke ambaye una kiwango kikubwa cha protini hii ya CYP2E1 katika matiti yako na unakunywa pombe basi utakuwa kwenye hatari kubwa ya kupata saratani ya matiti ikilinganishwa na mwanamke ambaye ana kiwango kidogo cha protini hii katika matiti yake.” Aliendelea kusema Profesa Maria de Lourdes Rodriguez-Fragoso.
Uchunguzi uliofanywa kutoka kwenye tishu za matiti ya wanawake wenye afya njema ambao wamefanyiwa upasuaji wa kukuza matiti yao umeonyesha viwango tofauti vya protini hii katika wanawake hawa.
“Hii inamaanisha ya kwamba wanawake wanatafautiana kwa umengenywaji wa pombe na hivyo inabidi kila mwanamke kuchukua hatua tofauti katika kupunguza uwezekano wa kupata saratani ya matiti” Alisema tena Profesa Maria de Lourdes Rodriguez-Fragoso.
Protini hii ya aina ya CYP2E1 hupatikana katika seli za matiti ya mwanamke zinazojulikana kama mammary epithelial cells ambapo pia ndio chanzo cha seli/chembechembe nyingi za saratani ya matiti na kusababisha watafiti hao kuanza kushuku uhusiano wake na saratani ya matiti.
Ili kuthibitisha shauku yao kwamba protini hii husababisha saratani ya matiti, watafiti hao walichukua tishu za matiti zilizo na viwango tofauti vya CYP2E1 na kuziweka kwenye pombe. Matokeo yalionyesha ya kwamba seli zenye kiwango kidogo cha protini aina ya CYP2E1 hazikuathiriwa sana ikilinganishwa na seli ambazo zilikuwa na kiwango kikubwa cha protini hiyo.
Utafiti huu ni ushindi mkubwa katika vita dhidhi ya saratani ya matiti kwani utasaidia kupunguza kiwango cha saratani hii kwa wanawake

0 comments:

Post a Comment