Tuesday 18 September 2012

SIMU ZA MKONONI NA KANSA YA UBONGO: BALAA JINGINE KWA AFRIKA?

Kwa muda mrefu kumekuwa na mjadala mkali kuhusu nguvu za mionzi ya mnunurisho inayotolewa na simu za mkononi kama zinaweza kusababisha kansa ya ubongo ama la. Hatimaye Shirika la Afya Duniani limetoa tamko kuhusu utafiti unaoonyesha kwamba simu za mkononi zinaweza kuwa zinasababisha kansa ya ubongo. Hatari hii inasemekana kuwa ni kubwa zaidi kwa watoto wadogo na matineja kwani mafuvu yao bado hayajakomaa sawasawa. Naomba hii isiwe kweli kwani kama tunavyojua, Afrika ndiyo jalala la bidhaa feki, mbovu na zilizoisha muda wake. Bila shaka nitakuwa sahihi nikisema kwamba simu zinazotoa mionzi hatarishi kwa binadamu na zitakazokuwa zimepigwa marufuku sehemu zingine za dunia ndizo zitarundikana Afrika. Kama utafiti huu ni wa kweli basi miongo kadhaa tu ijayo Afrika itakumbwa na mripuko wa kansa ya ubongo – mojawapo ya kansa hatari kabisa na inayohitaji tiba ghali sana! Tunachoweza kufanya kwa sasa ni kufuata mapendekezo yaliyotolewa yakiwemo kununua simu zisizotoa mionzi mikali zaidi, kuweka simu mbali na sikio wakati wa maongezi na kwa wenye uwezo kununua vifaa vinavyosafirisha mawimbi ya sauti kama “Bluetooth”. Vifaa hivi huwekwa sikioni na vinaweza kudaka mawimbi ya sauti ya simu iliyowekwa mfukoni au sehemu nyingine na kuyasafirisha sikioni kwa msikilizaji bila madhara yo yote.

0 comments:

Post a Comment