Tuesday 25 September 2012

Watanzania mabingwa wa kiswahili?

Kwa mpenzi yeyote wa Kiswahili ni sharti azingatie stadi nne za lugha hiyo. Yaani kuzungumza, kusoma kuandika na kuelewa lugha ya Kiswahili. Hata hivyo baadhi ya wakenya wamekuwa wakilamika kuwa vitabu vingi vya Watanazani vimekuwa vikitahiniwa nchini Kenya hususan katika vidato vya tatu na vinne. Ukweli ni kuwa Watanzania wamewabwaga wakenya na ipo mifano ya kutajika kuhusiana na hilo katika vitabu hususan vya fasihi. Swali ni je Wakenya wamepewa fursa ya kuandika au la? Ni nani anastahili kuwaambia waandike vitabu vya Kiswahili, na je wachapishaji vitabu wako radhi kuzichapisha kazi za Wakenya? Kuanzia miaka ya themanini hadi sasa, idadi ya vitabu vya Watanzania vilivyotahiniwa katika kunga za riwaya, tamthilia na ushairi ni kubwa kushinda vya Wakenya. Riwaya ya Kusadikika ya Shaaban Robbert(Mtanzania) ilitahiniwa mwanzoni mwa miaka ya tisini hadi mwaka 1994. Wakati huo hadi mwaka 1997 tamthilia ya Mashetani ya Ebarahim N. Hussein(Mtanzania) ilitahiniwa. Mwaka wa 1994 hadi mwaka 1998 riwaya ya Kisima cha Giningi ya Mohamed Said Abdullah(Mtanzania) ilitahiniwa. Katika miaka hiyo kuanzia mwaka 1998 tamthilia ya Amezidi ya Said Ahmed Mohamed (Mpemba) ikaanza kutahiniwa kuchukua mahali ya tamthilia ya Buriani ya A. S Yahya na David Mulwa(Wakenya). Wakati huo Mkenya Khaemba Ongeti alijipenyeza na tamthilia yake ya Visiki. Hayakuishia hapo, baada ya tamthilia za Visiki na Amezidi kuondolewa katika ratiba ya shule za upili nchii Kenya ikaingia riwaya nyigine ya Mohamed Said Ahmed (Mpemba) ya Kitumbua kimeingia mchanga. Na hiyo ilipoondoka ikaja riwaya ya Utengano ambayo inatahiniwa hadi sasa. Ukweli unaojitokeza hapa ni kuwa taasisi ya elimu nchini haiviteui vitabu hivyo kwa sababu ni vya Watanzania. Ni kutokana namna vilivyosukwa kimaudhui na kifani.Isitoshe waandishi wa vitabu hivyo wameandika wameandika vitabu vingi tu. Kwa mfano Said Ahmed Mohemed ameandika zaidi ya vitabu 40 vya Kiswahili. Mohamed Said Abdullah ameandika vitabu vingi tu kama vile Kisima cha Giningi, Duniani kuna watu, Mizimu ya watu wa kale na Kadhalika. Hata hivyo ni vyema kutambua kuwa baadhi ya Wakenya wamejitokeza na kuandika kazi nzuri za fasihi ya Kiswahili kama vile Siku Njema ya Ken Walibora, Mstahiki Meya ya Timothy Arege na Kifo Kisimani ya Kithaka Wamberia. Kwa ufupi wapenzi wa Kiswahili katika kanda ya Afrika Mashariki wakijumuisha mataifa ya Rwanda, Sudan Kusini, Sudan, Somalia na Uganda waandike vitabu zaidi vya Kiswahili. Twasubiri siku watanzania watavitahini vitabu vya Kiswahili vya wakenya, Vivyo hivyo si dhambi kitabu cha Kiswahili kilichoandikwa na Mrundi ama Mnyarwanda kikitahiniwa Uganda na vinginevyo. Ni maoni tu!!!!

0 comments:

Post a Comment