Wizara ya Nishati na Madini, imeagiza biashara ya madini ya
Tanzanite, ifanyike katika Halmashauri ya Simanjiro na siyo Arusha na Moshi
kama inavyofanyika hivi sasa.
Naibu Waziri wa wizara hiyo Dk Medard Kalemani, alitoa agizo
hilo mjini Babati kama njia mojawapo ya kuhakikisha ulipaji wa kodi na kudhibiti
utoroshwaji wa madini hayo, yanapatikana eneo la Mirerani, wilayani Simanjiro
pekee.
Alikuwa akizungumza na wachimbaji wakubwa na wadogo, pamoja
na wanunuzi, katika kikao kilichofanyika ukumbi wa Mkoa wa Manyara Jumamosi
iliyopita.
Alisema haiingii akilini kuona wananchi wa Wilaya ya
Simanjiro wakiishi katika hali ya kukosa mahitaji ya lazima kama maji safi,
shule zilizokamilika na badala yake wananchi kuwa katika maisha duni ilhali
wilaya hiyo ina utajiri mkubwa, badala yake wanufaika wa madini hayo ni
watoroshaji na wananufaisha nchi nyingine.
Mkuu wa Wilaya ya Simanjiro, Zephania Chaula, alisema wilaya
hiyo ina wachimbaji wa madini zaidi ya 2,000 ambao hawalipi kodi, na kwamba
halmashauri ya wilaya hiyo inapoteza mapato mengi kwa kuwa fedha inayopata
inatokana na mchanga wa madini na si madini yenyewe.
0 comments:
Post a Comment