Thursday 29 June 2017

DPP ASUBIRI FAILI LA LOWASSA……….

Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP), Biswalo Mganga, amesema anasubiri Ofisi ya Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI) imalize uchunguzi wake dhidi ya tuhuma zinazomkabili Waziri
Mkuu wa zamani, Edward Lowassa.
Lowassa ambaye pia ni mjumbe wa Kamati Kuu Chadema, alihojiwa juzi kwa DCI kwa tuhuma za kutoa maneno ya uchochezi na kuandika maelezo ya onyo.
Alijidhamini mwenyewe na leo anatakiwa kurudi tena katika ofisi hizo.
Akizungumza na mwandishi wa habari hii Mganga alisema kwa sasa hawezi kusema lolote kwa sababu DCI bado anaendelea na uchunguzi wa suala hilo.
Alikuwa akijibu swali aliloulizwa kuhusu uchunguzi unaoendelea dhidi ya Lowassa na kama atafikishwa mahakamani iwapo itabainika kuna jinai. Mganga alisema kuwa hawezi kufanya kazi kwa hisia ila anasubiri kuona nini kitatokea katika suala hilo.
Wakati DPP akieleza hayo, leo Lowassa ametakiwa kurejea tena katika Ofisi ya DCI kujua hatima yake kama ana kesi ama la.
Lowassa anadaiwa kutoa maneno ya uchochezi Ijumaa iliyopita wakati wa futari iliyoandaliwa na Mbunge wa Ukonga, Mwita Waitara (Chadema).

Alikaririwa na vyombo vya habari akisema kuwa ni jambo la fedheha kwa nchi kuwaweka mahabusu masheikh wa Jumuiya ya Uamsho na Mihadhara Zanzibar (Jumuki) maarufu Uamsho kwa miaka minne bila kesi kuamuriwa. Akizungumza na waandishi wa habari juzi baada ya kutoka polisi, Lowassa alisema baadhi ya watu waliitafsiri kauli aliyoitoa wakati wa futari hiyo kwamba ni ya uchochezi. Alisema kwa mtazamo wake hakuna kosa alilofanya na kwamba alikuwa anatekeleza sera ya chama chake. 

0 comments:

Post a Comment