Thursday 29 June 2017

MAITI TATU 3 ZAOKOTOWA KWENYE VIROBA...

Maiti tatu zimeokotwa kwenye fukwe mbalimbali za Zanzibar katika siku tatu zilizopita zikiwa zimeharibika vibaya, kuwa na majeraha ya kukatwa na kitu chenye makali zikiwa zimefungwa kwenye
viroba
Maiti ya mwisho iliokotwa jana katika ufukwe wa bahari wa Mtende, Mkoa wa Kusini Unguja ikiwa na majeraha na kufungwa katika kiroba. Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kusini Unguja, Juma Sadi, amesema kuwa mwili huo ulikuwa umeharibika vibaya hivyo kulazimika kuzikwa katika eneo hilo, kutokana na kutotambuliwa wala kuwa na nyaraka ama taarifa zozote za kuitambua maiti yake. Alisema mwili huo uliokotwa majira ya saa mbili asubuhi jana na wakazi wa eneo hilo ambao wanadhani kuwa ulisukumwa na wimbi la maji ya bahari kutoka eneo la mbali.
Alisema hiyo ni maiti ya tatu kukutwa katika fukwe za bahari katika mkoa huo katika siku tatu, baada ya mwili wa kwanza kuokotwa Jumatatu katika pwani ya Bungi na nyingine kukutwa katika ufukwe wa bahari ya Makunduchi juzi.

Alisema jeshi la polisi linaendelea na uchunguzi ili kupata taarifa kama kuna mtu aliyepotea ili kuhusisha na matukio hayo yanayofanana. Aidha, Kamanda Sadi aliitaka jamii kusaidia kutoa taarifa ya kupotelewa na jamaa au ndugu zao ili kulisaidia jeshi hilo kuharakisha upelelezi juu ya maiti hizo ambazo ni za wanaume wanaokadiriwa kuwa na umri kati ya miaka 35 hadi 40.

0 comments:

Post a Comment