Mahakama ya juu nchini Kenya imebatilisha uchaguzi wa urais nchini
humo baada ya kujiridhisha kuwa ulikuwa na kasoro nyingi zilizokiuka katiba na
utawala wa sheria.
Mahakama hiyo imesema kuwa
imeridhishwa na ushahidi uliowasilishwa na upande wa walalamikaji ambao ni
kambi ya NASA iliyokuwa imemsimamisha mgombea wake Raila Odinga, hivyo imeamuru
uchaguzi huo kufanyika upya.
Kati ya majaji saba
waliosikiliza kesi hiyo, majaji watano wameeleza kukubaliana na ushahidi wa
upande wa walalamikaji kuwa kulikuwa na ukiukwaji mkubwa wa sheria katika
uchaguzi huo uliofanyika Agosti 8 mwaka huu.
“Mlalamikiwa namba moja (Tume
Huru ya Uchaguzi) ilishindwa, ilipuuzia na ilikataa kuendesha uchaguzi kwa
misingi iliyoainishwa kwenye katiba,” hukumu hiyo imeeleza.
Imeeleza kuwa ukiukwaji mkubwa
wa katiba na udanganyifu ulifanyika wakati wa kuhamisha na kujumlisha kura kwa
njia ya kielektroniki.
Kwa mujibu wa katiba ya nchi hiyo, uchaguzi huo unapaswa kurudiwa
ndani ya siku 60 tangu uamuzi wa mahakama kutolewa.
Tume Huru ya Uchaguzi ya Kenya
ilimtangaza Uhuru Kenyatta kuwa mshindi wa uchaguzi huo akimshinda kwa mbali
mpinzani wake, Raila Odinga.
Hii ni mara ya kwanza kwenye
historia ya Afrika kwa Mahakama kufuta uchaguzi wa urais uliofanyika tangu
kuanzishwa kwa mfumo wa vyama vingi ndani ya bara hilo.
0 comments:
Post a Comment