Wednesday 4 November 2015

Wapiga kura wakataa kuhalalisha bangi Ohio....!!

Wapiga kura katika jimbo la Ohio nchini Marekani, wamekataa pendekezo la kuhalalisha matumizi ya bangi katika jimbo hilo.

Pendekezo hilo lililopewa jina Issue 3, lingefanyia marekebisho sheria ya jimbo la Ohio na kuifanya bangi kuwa halali kwa raia yeyote aliye na umri wa miaka 21 na zaidi, kuitumia kwa sababu za kibinafsi na za kimatibabu.
Kuhalalishwa kwa bangi kungewezesha bidhaa zilizotiwa bangi, kama vile peremende kuuzwa madukani.
Raia wa kawaida pia wangeruhusiwa kukuza hadi mimea minne ya bangi majumbani.
Lakini kwa mujibu wa makadirio ya kura yaliyofanywa na vyombo vya habari jimboni humo, pendekezo hilo limeshindwa na kiwango cha kura mbili kwa moja.
Makundi yaliyotetea kuhalalishwa kwa bangi yalitumia hadi $12m kwenye matangazo kabla ya kura hiyo kupigwa Jumanne.
Sheria ya Issue 3 ingetoa idhini kwa bangi kukuzwa katika maeneo 10 jimbo la Ohio, jambo ambalo wakosoaji wanasema lingepelekea kuwepo kwa ukiritimba.
Kambi ya waliotetea sheria hiyo ilikuwa na watu mashuhuri wakiwemo msanii Nick Lachey, na Woody Taft, ambaye ni ndugu wa rais wa zamani wa Marekani William Howard Taft.
Pendekezo hilo lilipingwa vikali na hospitali zinazoshughulikia watoto, baadhi ya mashirika ya kibiashara na wakulima.
Majimbo ya Colorado, Washington, Oregon na Alaska, pamoja District of Columbia, yamehalalisha matumizi ya bangi kwa sababu za kujiburudisha.

Majimbo 20 nayo huruhusu matumizi ya bangi kwa sababu za kimatibabu.

0 comments:

Post a Comment