Gereza la
Songwe mkoani Mbeya linatarajiwa kuvunjwa na kujengwa sehemu nyingine kupisha
uchimbaji wa madini adimu duniani ya niobium.
Ni baada
ya madini hayo kugundulika kuwapo kwenye eneo la gereza hilo,endapo utaanzishwa
mgodi wa madini hayo utakuwa wa pili katika Bara la Afrika baada ya Nigeria.
Taarifa za
uhakika zimeonyesha michoro ya ujenzi wa gereza jipya imeandaliwa.
Mhandisi
wa Migodi wa Kanda ya Kusini Magharibi, Zephania Nsungi alisema Kampuni ya
Panda Hill Niobium Project Tanzania imefanikiwa kupata madini hayo karibu na
gereza hilo.
Madini hayo
ni adimu duniani na yanapatikana katika nchi chache sana, hivyo yakianza
kuchimbwa upo uwezekano wa kuliondoa Gereza la Songwe na kujengwa upya eneo
jingine.
Mfanyakazi
wa kampuni hiyo Emmanuel Kisasi alisema kwamba, viongozi wao wako likizoni
Ulaya na wanatarajia kurejea nchini mwezi ujao.
Kisasi
ambaye hakutaka kuzungumza kwa kina juu ya madini hayo, alithibitisha kuwapo
kwa mpango wa kuanza kwa mgodi eneo hilo na kwamba, unatarajiwa kudumu kwa
zaidi ya miaka 30.
Mkuu wa
Magereza mkoani humo Julius Sang’udi naye alithibitisha kuwapo kwa mpango huo
na kusisitiza kwamba, unasimamiwa na Wizara ya Nishati na Madini kwa
kushirikiana na Jeshi la Magereza chini ya Kamishna aliyemtaja kwa jina moja la
Chamlesile.
Kwa mujibu
wa taarifa za mtandao, madini hayo huchanganywa na metali zingine na vyuma
vyake hutumika kwenye ujenzi wa bomba la kupitishia mafuta.
Vilevile
hutumika kama metali kwa injini za ndege na husaidia kuzuia mitambo yake
kutopata joto kali.
0 comments:
Post a Comment