Thursday 22 March 2018

WAZIRI ASIMAMISHWA KAZI KWA KUMPIGA MBUNGE…

Bunge la Zambia limemsimamisha kazi Waziri wa Jimbo la Lusaka Bowman Lusambo kwa muda wa mwezi mmoja, baada ya kumchapa kibao mbunge Chishimba Kambwili wakiwa bungeni.


Spika wa Bunge hilo amesema ni jambo la kawaida wabunge kutumia lugha isiyofaa na kuleta mizozo, lakini kwa kitendo cha Waziri kumpiga kibao mbunge ni kitendo kisicho vumilika.

Patrick Matibini ambaye ni spika wa Bunge hilo, amesema kitendo hicho kilifanyika Oktoba mwaka jana na kuongezea kwamba tabia hiyo haikubaliki kamwe.

Kufuatia adhabu hiyo Waziri Lusambo atasitishiwa baadhi ya huduma zinazotolewa bungeni kama marupurupu na mshahara, kwa muda wa kipindi chote atachokuwa anatumikia adhabu hiyo.

Aidha imeelezwa kuwa mbunge huyo aliyepigwa kibao amekuwa akiwatukana maofisa wa Serikali kwa tuhuma za rushwa tangu atolewe kuwa Waziri wa Mawasiliano mwaka 2016, japo Serikali imekuwa ikikanusha tuhuma hizo.


Hata hivyo imeelezwa kuwa Waziri huyo alichukua sheria hiyo mkononi ya kumchapa kibao mara mbili baada ya kuona mbunge huyo anazungumza uongo juu ya Serikali.

0 comments:

Post a Comment