Monday 21 September 2015

Magari ya Volkswagen yachafua mazingira…

Mkurugenzi mkuu wa kampuni ya magari ya Volkswagen, ameomba msamaha baada ya wasanifu nchini Marekani kusema baadhi ya magari yake yamekuwa yakichafua mazingira.

''Naomba msamaha mimi mwenyewe kwamba tumevunja heshima kwa wateja wetu na umma kwa jumla'', alisema Winterkorn.
Ameanzisha uchunguzi dhidi ya kifaa kilichowekwa katika magari hayo,ili kupunguza hewa chafu wakati wa ukaguzi ikilinganishwa na wakati gari hizo zinapoendeshwa.
Hisa za kampuni hiyo zilishuka kwa asilimia 18 zilipoanza biashara.
Kampuni hiyo ya magari nchini Ujerumani, ilishinikizwa kurudisha magari yake nusu milioni siku ya ijumaa.
Idara ya mazingira ilipata kifaa hicho katika magari ya Audi A3, VW jetta, Beetle, Golf na yale ya aina ya Passat.
Mbali na kuyarudisha magari hayo kwa ukarabati, kampuni hiyo pia itakabiliwa na faini za mabilioni ya madola.
Huenda wakuu wa kampuni hiyo pia wakashtakiwa na mashtaka ya uhalifu.
Shirika hilo la mazingira linasema kila gari ambalo halikuzingatia sheria ya hewa safi itapigwa faini ya dola elfu 37 na mia 5.

Huku magari laki 4 na elfu 82 yakiwa yameuzwa tangu mwaka 2008, huenda faini hizo zikafika dola bilioni 18.

0 comments:

Post a Comment