Wabunge na maseneta walivalia mavazi yanayofanana na sare za wanafunzi |
Baadhi
ya viongozi wa upinzani nchini Kenya wamevalia mavazi yanayofanana na sare za
wanafunzi wakiitaka serikali kulipa walimu nyongeza ya mishahara.
Walimu wamekuwa mgomoni tangu
kufunguliwa kwa muhula wa tatu na Serikali ilifunga shule zote za umma
Jumatatu.
Mrengo wa Coalition for Reforms and Democracy (Cord)
unaoongozwa na Raila Odinga jana iliandaa mkutano wa kisiasa uwanja wa Uhuru
Park, Nairobi kuishinikiza serikali iwalipe walimu nyongeza ya asilimia 50 hadi
60 kama ilivyoagizwa na mahakama.
"Kuna pesa za kutosha,
lakini zinapotea kwa ufisadi. Uhuru (Rais Kenyatta) anafaa kushauriana na
walimu. Asiseme hawezi kulipa na hatalipa," alisema Bw Odinga.
Kiongozi wa chama cha Wiper
Kalonzo Musyoka alisema "pesa zipo" za kuwalipa walimu.
Mgomo huo wa walimu unatishia
kutatiza mitihani ya kitaifa ambayo inatarajiwa kuanza wiki chache zijazo.
Kwa mujibu wa Baraza
la Kitaifa la Mitihani Kenya (KNEC) kuna watahiniwa 937,467 wanaojiandaa
kufanya mtihani wa darasa la nane KCPE utakaoanza Novemba 10 na kumalizika
Novemba 12.
Watahiniwa wanaojiandaa kufanya mtihani wa kidato cha nne
KCSE utakaoanza rasmi Oktoba 12 ni 525,802.
Baraza hilo limesema mitihani
hiyo haitaahirishwa.
0 comments:
Post a Comment