Sunday 5 March 2017

POMBE ZA VIROBA ZENYE THAMANI YA BILIONI 10.8 ZAKAMATWA DAR…….

Pombe kali zilizofungashwa katika vifungashio vya plastiki  maarufu kama ‘viroba’ zenye thamani ya shilingi Bilioni 10.8 zimekamatwa Jijini Dar es Salaam katika msako wa pombe hizo uliofanyika kuanzia Machi 01 mpaka 03, mwaka huu.

Hayo yamesemwa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) January Makamba,  mapema hii leo Jijini Dar es Salaam alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari kuhusu operesheni ya utekelezaji wa maelezo ya Serikali ya kusitisha pombe hizo za viroba hapa nchini kuanzia Machi 01, mwaka huu.
“Jumla ya katoni 99,171 za pombe kali zilizofungashwa kwenye vifungashio vya plastiki (Viroba) zimekamatwa ambapo katoni 69,045 ni zenye ujazo wa  na mililita 50, katoni 29,344 zenye ujazo wa mililita 100, katoni 782 zenye ujazo wa mililita 90 pamoja na katoni 10,625 za chupa zenye ujazo wa mililita 100. Thamani yake ni Shilingi Bilioni 10.83,” amesema Makamba.
Aidha, amesema kuwa, jumla ya viwanda 16 vya kuzalisha pombe kali, maduka ya jumla 18, maghala 4, baa 3 na kiwanda kimoja cha kuzalisha bidhaa za plastiki ikiwemo vifungashio vya plastiki vya kufungashia viroba vilikaguliwa katika opesheni hiyo.
Vile vile amesema kuwa, pombe zilizokamatwa zimezuiliwa kuuzwa  au kusambazwa kutoka katika maeneo ambayo yamehifadhiwa yaani viwanda, maghala pamoja na maduka ya jumla mpaka hapo Serikali itakapotoa tamko.
Hata hivyo, Makamba amesema kuwa zawadi kati ya shilingi laki 5 hadi milioni 1 zitatolewa kwa mwananchi atakayetoa taarifa itakayowezesha kukamatwa na kushtakiwa kwa mtu yeyote mwenye ghala au aliyehifadhi shehena ya pombe za viroba kinyume cha sheria, watu au mtu anayeingiza  pombe za viroba nchini kutoka nje ya nchi kinyume na sheria na utaratibu, anayehamisha au kusafirisha pombe za viroba kinyume na sheria, mtu mwenye kiwanda/mtambo wa kuzalisha pombe za viroba ambao hautambuliki na Serikali pamoja na mtu anayetumia stempu feki za TRA .

0 comments:

Post a Comment