Leo tarehe 8 Machi, 2017 dunia
zima inaadhimisha Siku ya Wanawake Duniani, ambayo huadhimishwa kila mwaka kwa
lengo la kutambua na kuthamini mchango wa mwanamke katika jamii. Chimbuko
la kuanzishwa kwa Siku ya Wanawake lilianza mwanzoni mwa
miaka ya 1900 kufuatia
maandamano ya wanawake wafanyakazi wa sekta ya viwanda nchini Marekani kupinga
mazingira duni ya kazi.
Waandamaji hao, walilalamikia
ukosefu wa huduma za kijamii na kuwepo kwa vitendo vya unyanyasaji katika ajira
ikiwemo wanawake kulipwa mshahara mdogo kwa kazi sawa ukilinganisha na wanaume.
Kwa kuzingatia hali hiyo, Umoja
wa Mataifa baada kuanzishwa mwaka 1945 uliridhia kuwa tarehe 8 Machi kila mwaka
iwe ni Siku ya Kimataifa ya Wanawake Duniani.
Uamuzi wa Umoja wa Mataifa wa
kuanzisha Siku ya Wanawake Duniani ulitokana na ukweli kwamba masuala ya haki,
maendeleo na usawa wa wanawake yalihitaji msukumo maalumu na wa kipekee.
Lengo kuu la kuadhimisha Siku
ya Wanawake Duniani ni kutoa fursa kwa jamii kupima utekelezaji wa maazimio,
matamko, mikataba na itifaki mbalimbali za Kimataifa, kikanda na kitaifa
zinazohusu masuala ya maendeleo ya jinsia na uwezeshaji wanawake.
Hii ni pamoja na kuhakikisha
kuwa haki za wanawake kiuchumi, kijamii, kiutamaduni na kisiasa zinapatikana na
zinalindwa.
Kuadhimisha Siku ya Wanawake
Duniani ni kuhamasisha jamii kuhusu umuhimu wa kutambua na kuthamini uwezo na
mchango mkubwa wa wanawake katika kuleta maendeleo pamoja na kuelezea jitihada
mbalimbali zilizofanywa na Serikali na wadau mbalimbali katika kuwajengea uwezo
wa kiuchumi na kijamii ili waweze kushiriki kikamilifu katika kujiletea
maendeleo yao, familia zao, jamii na Taifa kwa ujumla.
Kwa Tanzania wanawake ni kundi
kubwa na muhimu katika jamii (asilimia 51 ya Watanzania Wote) hivyo hakuna
maendeleo yeyote yanayoweza kufikiwa ikiwa kundi hili litaachwa nyuma.
0 comments:
Post a Comment