Wednesday 22 June 2016

STAILI YA UKAWA YABAMBA MITANDAONI…!

Picha za watu wa kada mbalimbali nchini wakiigiza ‘staili’ mpya ya wabunge wa
Ukawa waliojibandika karatasi midomoni zenye ujumbe tofauti kuhusu haki ya uhuru wa Bunge wanayodai kuminywa na Naibu Spika, Dk Tulia Ackson zimeiteka mitandao ya kijamii nchini.
Tukio la wabunge hao lilitokea juzi mjini Dodoma ikiwa ni mwendelezo wa siku 17 za kususa vikao vinavyoongozwa na Dk Tulia tangu akatae kujadili hoja ya kusimamishwa wanafunzi 7,802 wa stashahada maalumu ya sayansi katika Chuo Kikuu cha Dodoma (Udom), wiki tatu zilizopita.
Kama ilivyokuwa kwa wabunge hao watu mbalimbali wanapiga picha za kuigiza tukio hilo na kuziweka katika mitandao ya facebook, twitter na Instagram, baadhi wakiandika ujumbe kwenye karatasi wanazobandika midomoni ama wakiwaponda Ukawa au wakiwaunga mkono.
Mbali na waliobandika karatasi midomoni, wengine waliamua kujiziba kwa nguo, vilemba huku baadhi wakitumia kadi za CCM na Chadema na kuweka ujumbe wa kukosoa au kupongeza tukio hilo huku wengine wakitumia neno ‘kuziba mdomo’ kutoa yao ya moyoni ambayo hayahusiani na kitendo cha wabunge wa Ukawa.

Tukio hilo lilivuta wafuatiliaji wengi katika mitandao hiyo, katika ukurasa wa facebook wa gazeti la mwananchiNews, watu 255,372 walifungua picha za wabunge hao wa Ukawa huku watu 922 wakizinakili na kuzituma katika kurasa zao za mtandao.

0 comments:

Post a Comment