Wanaume wanaoishi na virusi vya Ukimwi sasa huenda wakapata
suluhisho, la kupata
watoto na wenza wao ambao hawana virusi hivyo, baada ya
kuwapo tiba ya kusafisha mbegu za kiume zenye VVU hapa nchini.
Tiba hiyo sasa inapatikana hapa
nchini katika hospitali moja iliyo jijini Dar es Salaam, ambayo inatoa huduma
za uzazi na upandikizaji wa mimba katika mirija ya uzazi kitaalamu inayojulikana
In Vitro Fertilization (IVF).
Kwa sasa, njia ya kuzuia maambukizi
ya VVU kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto (MTCPT) ndiyo inayotumika duniani kote,
kwa mjamzito kupewa dawa za ARV wakati wa ujauzito zinazokinga maambukizi
kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto na baada ya mtoto kuzaliwa.
Kadhalika mtoto hutakiwa kunyonya
maziwa ya mama pekee kwa kipindi cha miezi sita au kutonyonya kabisa ili
asipate maambukizi.
Tovuti ya hospitali inayotoa huduma
hizo, inaeleza kuwa wanatoa huduma hiyo ya kusafisha mbegu za kiume zenye VVU
na kisha kuzipandikiza kwa mwanamke asiye na VVU kwa njia ya IVF.
Shirika la Afya la Kimataifa (WHO),
liliwahi kuchapisha utafiti wa kuosha mbegu za kiume na kueleza kuwa matibabu
hayo yanawezekana, ingawa si kwa asilimia 100.
Katika utafiti wa WHO, wenza 914
walipimwa baada ya mbegu za kiume kuoshwa. Kati ya hao, wanawake walipopimwa
baada ya kupata ujauzito hawakuonekana na VVU, wala watoto hawakuonekana kuwa
na maambukizi hayo.
Kadhalika WHO walieleza kuwa matokeo
ya utafiti huo yalionyesha kuwa kati ya asilimia 1 hadi 20 ya mbegu zilizooshwa
na kupandikizwa kwa wanawake, bado zilikuwa na VVU. (yaani kesi 70 kati ya
sampuli 1279)
Wanasema mbinu hiyo ya kusafisha
inahusisha mchakato mrefu, ikiwamo kupima zaidi ya mara kumi sampuli za mbegu
zilizosafishwa.
Hata hivyo WHO wamesema kuosha mbegu za kiume kunapunguza hatari ya
maambukizi, lakini hakuwezi kuondoa kabisa VVU ndani ya mbegu hizo.
Hospitali
Tovuti ya kliniki hiyo inaeleza wazi
huduma zinazotolewa ambapo mbali na uchangiaji wa mbegu na mayai, lakini huduma
kuu ni kuwasaidia wenye matatizo ya uzazi, kupata watoto kwa njia ya
upandikizaji.
Huduma nyingine ni kutibu matatizo ya
ugumba kwa wanawake na wanaume, kuchagua jinsia ya mtoto, upasuaji wa kukaza
kizazi kuzuia mimba kutoka (shridkar shuture) pamoja na huduma za uzazi.
Kuchangia mbegu au mayai ni katika
kuhakikisha hakuna upungufu wa mbegu, na kuwasaidia wale wote ambao wameshindwa
kutimiza ndoto za kuwa na familia.
Jinsi mbegu zinavyooshwa
Kisayansi, damu pekee si kipimo cha
kuonyesha kuwapo kwa maambukizo ya VVU katika mwili bali hata katika majimaji
ya mwilini.
Ogani zinazozalisha majimaji ya mbegu
za kiume, huathiriwa kwa namna ya pekee na VVU.
Daktari Bingwa wa Uchunguzi wa
magonjwa, Henry Mwakyoma alisema kwa kawaida virusi vya Ukimwi hupenda kukaa
katika chembehai nyeupe(CD4).
Alisema ndiyo maana inawezekana
mwanamume mwenye VVU, asimwambukize mwenza wake.
Hata hivyo, Dk Mwakyoma aliona kuna
ugumu kuzisafisha mbegu za kiume na kuondoa majimaji yake yenye VVU, ili
kuzipandikiza mbegu hizo ili zitungishe mimba kama unavyosema utafiti huo.
Daktari wa Kitengo cha Uchunguzi wa
magonjwa katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili, Innocent Mosha anaungana na Dk
Mwakyoma na kusema, kwa kawaida mbegu za kiume hazina VVU kwa sababu ni seli
inayojitegemea, lakini majimaji yanayobeba mbegu hizo ndiyo huwa na VVU.
Wanasayansi wanasema mwanamume
anaweza asionyeshe VVU katika damu, lakini majimaji ya mbegu za kiume
yakaonyesha uwapo wa virusi.
Wanaeleza kuwa kwa mwanamume
anayetumia dawa za kufubaza makali ya VVU, majimaji hayo yakipimwa hayaonyeshi
uwapo wa VVU, bali virusi huonekana katika damu tu. Hii ni kwa sababu ARV
hupunguza wingi wa virusi na hivyo kushuka na kufikia kiwango cha kutoonekana.
Jarida la Science Daily la nchini
Uingereza linaonyesha robo tatu ya wanaume wanaoishi na VVU na wanaotumia ARV,
walipopimwa majimaji yanayobeba mbegu za kiume hayakuwa na VVU.
Hata hivyo, utafiti uliofanywa mwaka
2009 na Jarida la Tiba la nchini Canada ulibaini kuwa mbegu za kiume zina
nafasi kubwa ya kusambaza virusi vya Ukimwi.
Utafiti huo ulikinzana na huu wa
usafishwaji wa mbegu hizi, kuondoa majimaji ambayo kwa kawaida ndiyo hudhaniwa
kubeba VVU.
Matokeo ya utafiti huo yalionyesha
kuwa mbegu za kiume zina nafasi kubwa ya kusambaza VVU wakati wa tendo la ndoa,
kwani virusi hivyo hujichimbia katika chembehai nyeupe ambazo utafiti ulisema
ipo katika mbegu za kiume.
Utafiti huo ulikanusha tafiti za awali
ambazo zinathibitisha kuwa ni majimaji tu yanayobeba mbegu hizo ndiyo yenye
kuathiriwa na VVU.
Source Mwananchi news Paper
0 comments:
Post a Comment