Friday 6 May 2016

WATUMIAJI SIMU FEKI WAZIDI KUPUNGUA…

Kadri siku ya kuzima simu feki kote nchini inavyokaribia, imebainika kuwa wanaozitumia wanazidi kupungua nchini.

Meneja Mawasiliano wa Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Mawasiliano Tanzania (TCRA) Innocent Mungy, amesema tangu ilipotangaza mwaka jana kuwa itazima simu feki ifikapo mwishoni mwa Juni, idadi ya watumiaji imepungua kutoka asilimia 30 hadi 13.
Amesema wakati wa uhakiki wa matumizi ya simu feki Desemba mwaka jana, mamlaka hiyo ilibaini kuwapo asilimia 30 ya simu bandia zinatotumika nchini.
TCRA ilifanya uhakiki mwingine Februari mwaka huu, ambao ulibaini matumizi ya simu feki kupungua hadi asilimia 18.
Amesema wananchi wamekuwa na mwitikio huo kwa sababu mamlaka hiyo imekuwa ikitoa elimu kote nchini juu ya matumizi ya simu hizo.
Hadi sasa TCRA imeshatoa elimu kuhusu wananchi kuacha kutumia simu feki, katika Kanda ya Kaskazini, Nyanda za Juu Kusini na Kanda ya Kati na wiki ijayo mamlaka hiyo itakuwa Kanda ya Ziwa.
Amesema Mkoa wa Dar es Salaam ambao una watumiaji wengi wa simu feki, utakuwa wa mwisho kupatiwa elimu hiyo, Juni kabla ya kuzima simu hizo.
Kuhusu watu wanaoweka namba feki za utambulisho (IMEI) kwenye vifaa vya elektroniki, amesema wanafanya kazi bure kwa sababu hata hizo zitazimwa siku ikifika.
Amesema hata mtu akibadilisha namba ya IMEI halisi kwenye siku feki, siku ya kuzima simu feki itazima tu.

Pia amesema ni vigumu kuwagundua watu wanaofanya ujanja huo kwa sababu wanapokuwa wanazibadilisha simu inakuwa imezimwa.

0 comments:

Post a Comment