Mganga Mkuu wa Wilaya ya Singida Vijijini, Dk. Erick
Bakuza ameandika barua ya kuacha kazi
Dk. Bakuza amechukua uamuzi huo ikiwa ni siku chache tangu
alipopewa adhabu ya kuwekwa mahabusu na Mkuu wa Mkoa huo, Dk. Rehema Nchimbi.
Dk. Nchimbi alitoa amri ya kukamatwa kwa daktari huyo kutokana
na kuzuka ugonjwa wa kipindupindu ambao ulisababisha vifo vya watu wawili
mwishoni mwa mwaka jana.
Mkurugenzi
wa Manispaa hiyo, Rashid Mandoa jana alithibitisha kuacha kazi kwa Dk. Bakuza.
“Ni kweli amewasilisha barua ya kuacha kazi lakini ninavyojua
mimi si kweli kwamba ameacha kazi kutokana na adhabu aliyopewa na Mkuu wa Mkoa
ya kuwekwa ndani.
“Kwanza ujue hakuwekwa ndani, na ameamua kuacha kazi kwa sababu
amepata sehemu nyingine ambayo anaona ina maslahi anayohitaji yeye,” alisema.
Juhudi za kumpata Dk. Bakuza kuzungumzia hatua yake hiyo
hazikuzaa matunda.
Kauli ya Mkuu wa Mkoa
Wakati Mkurugenzi huyo akisema kwamba Dk. Bakuza hakuwekwa
ndani, Mkuu wa Mkoa huyo, Dk. Nchimbi alithibitisha kwamba aliwekwa ndani
kwa saa tatu.
“Mimi nilitoa amri ya kukamatwa Daktari huyu na aliwekwa chini
ya ulinzi kwa saa tatu.Nilimuweka ndani kwa sababu ya mazingira ambayo
niliyakuta nilipokuja kuanza kuitumikia nafasi niliyoteuliwa ya ukuu wa mkoa,
na nitatetea uamuzi wangu huo.
“Niliamuru akamatwe kwa sababu ya mlipuko wa ugonjwa wa
kipindupindu, kesi ya kwanza ya kuwapo kwa mgonjwa wa kipindupindu iliripotiwa
Novemba 26, mwaka jana.
“Utaratibu unajulikana wazi kwamba ikifika kesi tano DMO (Mganga
Mkuu wa Wilaya) anatakiwa atoe taarifa kwa MRO (Mganga Mkuu wa Mkoa).
“Desemba 4 hakutoa taarifa, ilipofika Desemba 16
vikatokea vifo viwili hakutoa taarifa hadi Desemba 18 ndipo akatangaza.
“Nikaona hakuwa makini katika kazi yake kwa sababu alipaswa
kutangaza mapema ili tuchukue hatua za kudhibiti ugonjwa huo na naamini hata
hivyo vifo visingetokea,” alisema.
Dk. Nchimbi alisema suala la kipindupindu halipaswi kuchukuliwa
kisiasa na kwamba lenyewe lipo kitaalamu zaidi.
“Kuna taratibu ambazo hufuatwa lazima tupate evidence ya kutosha,
watu wachukuliwe vipimo, yeye alinyamaza kimya. Wataalamu walipokwenda
kuchunguza wakagundua kuna kipindupindu kwenye wilaya yake,” alisema.
Aliongeza: “Kwa hali hiyo niliona hakuwa makini katika
kazi yake, hivyo nilitaka kumshtua tu awe makini, hakuwa makini.
“Katika hali ya kawaida angesema mapema tungechukua hatua
mapema, tungetibu maji, tungesafisha visima na hata vifo visingetokea,”alisema.
0 comments:
Post a Comment