Monday 30 January 2017

MAHARUSI WAFUNGA NDOA KWA KUTUMIA DOLA MOJA KENYA

Ushawahi kuona sherehe ya harusi isiyo na burudani wala mapochopocho na gharama husika haizidi dola moja?

Basi wiki hii, Wakenya, Wilson Mutura na Ann walitumia shilingi mia moja au dola moja tu kufunga ndoa.
Dola yenyewe ilitumika kununua pete mbili zilizogharimu shilingi mia moja.
Sherehe hiyo tulivu ilifanyika katika mtaa wa Kasarani, mjini Nairobi.
Walipoona kuwa uhusiano wao ulinoga kwa kudumu kwa zaidi ya miaka mitatu na kuwa ni heri waiweke iwe rasmi, Wilson Mutura na Ann Mutura walianza safari ya kufunga pingu za maisha. Lakini safari yenyewe ilikumbwa na changamoto za kifedha.
Kutokana na mazoea ya sherehe za kifahari nchini humo, wawili hao walipanga na kupangua sherehe hiyo kwa sababu hawakuweza kukusanya kiwango walicholenga cha dola mia tatu.
Wilson na Anne wamelipiwa fungate na kampuni ya Bonfire
Maombi yao kwa familia na marafiki kuwafanyia mchango, hayakutimizwa.
Hilo liliwafanya waahirishe sherehe hiyo mara tatu.
"Nilipozungumza na kakangu, aliniambia, kwa nini nijisumbue ilhali wengi wao hawakuhitaji sherehe ya harusi?" aliuliza.
Lakini baada ya muda, Bwana harusi, Wilson, hakuwa na la kufanya ila kumshawishi mpenzi wake kuhusu uwezo wake.
"Wilson aliponieleza hali yake, sikukataa. Mapenzi yetu yalizidi yote," anasema bi Harusi, Ann.
Ingawa walikuwa na uwezo wa kuishi kwa mtindo wa 'come we stay' uliomaarufu kwa vijana wengine ambapo wapenzi wanaishi pamoja bila kuoana, Wawili hao walikwenda kwa askofu Jasper Owach kutoka Kanisa la Community Christian worship centre mjini Nairobi kurasmisha harusi yao.
"Mapenzi yetu yalidumu kwa muda na ili kujistiri kutoka maovu baada ya kupata baraka ya wazazi, tuliamua kufanya mambo yetu rasmi," anasema Wilson.
Siku yenyewe ilipofika, bwana Harusi, Wilson aliwashangaza waumini baada ya kukimbia nje sherehe ikiendelea.
"Alitoka ghafla kununua pete ya harusi nilipokuwa naendelea na shughuli ya kuwafunganisha," alisema askofu Jasper Owach, ambaye aliongoza hafla hiyo.




Wilson alirejea na walipokuwa wanatamka kauli za ndoa, Wilson alitoa pete hizo zilizofungwa kwa gazeti na wakavikana pete.

0 comments:

Post a Comment