DUNIA inakimbia kwa kasi ya ajabu mno! Hii inadhihirishwa na mabadiliko mbaliambali ya mifumo ya maisha ya kila siku.
Kadri siku zinavyozidi kwenda, ndivyo utandawazi unazidi kujitangazia ushindi, kwani mambo mengi yanahamia mtandaoni tofauti na ilivyokuwa zamani.
Leo hii utaona unaweza ukaishi Tanzania lakini ukaweza kubukua kwenye vyuo vya kimataifa kama Chuo Kikuu cha Florida kilichoko nchini Marekani au hata kile cha Uholanzi, huku ukiendelea kufanya shughuli zako za kila siku kama kawaida.
Ni wazi kuwa njia hii ya kusoma mtandaoni imekuwa ni msaada mkubwa mno hasa kwa watu wanaokabiliwa na majukumu mengi.
Jambo la kufanya hapa ni kuhakikisha kuwa unakompyuta au chombo chochote kitakachokuwezesha kusoma vizuri pamoja na intaneti ya uhakika kwa maana ya mtandao.
Njia hii ya masomo imewasaidia watu wengi kuokoa gharama na hata muda, pia inakupa uhuru wa kufanya mambo yako mengine.
Elimu hii imekuwa kwa kasi ikilinganishwa na kipindi cha miaka 10 nyuma mfano kwa mataifa kama Marekani idadi ya wanafunzi wanaosoma kwa njia ya mtandao imepaa kufikia milioni sita kutoka milioni mbili.
Si wanafunzi pekee walioongezeka kwenye njia hii ya masomo, bali hata vyuo vya aina hii vimeongezeka ambapo sasa hivi nchini Marekani pekee kuna vyuo milioni 21; hii ikiwa na wastani wa mwanafunzi mmoja kwa vyuo vitatu.
Inamaanisha kuwa mwanafunzi anao uwezo wa kusoma kwenye vyuo vitatu. Pindi wanafunzi wanaposoma kwa njia ya mtandao na kuhitimu masomo yao mambo ya mahafali huwa hayapo.
Kama wewe ni miongoni mwa mnaovutiwa na njia hii ya kutaka kubukua kwenye vyuo bora vya majuu na bado unajishauri kwa kushindwa kujua kuwa ni chuo gani utaenda kusoma huku pia ukihofia labda unaweza ukatapeliwa kwa kujiunga na vyuo visivyo na sifa, hivyo kujikuta ukipoteza dola zako makala haya yatakuwa ni msaada mkubwa mno kwako.
Acha kubaki nyuma kwa kutojua ujiunge na chuo gani ili uweze kutimiza ndoto zako za kujiendeleza kitaaluma kwa njia ya mtandao, kwani hapa kuna orodha ya vyuo vikuu bora kwa utoaji wa elimu kupitia mtandao (online).
Orodha hii inajumuisha vyuo takribani 100 lakini ili kuokoa muda na kukupa nafasi ya kuamua, hapa kuna vyuo vikuu 10 ambavyo ni vyema ukaanza navyo kwa kuangalia kipi kitakufaa kujiunga nacho kwa mwaka huu.
Chuo kilichofanikiwa kushika nafasi ya kwanza kwenye orodha hii ni Penn State World Campus, hiki ni moja ya vyuo vinavyoheshimika duniani kwa kutoa elimu kwa njia ya mtandao ambapo mpaka sasa kinatoa masomo kwenye fani 120 huku kikijinyakulia jumla ya wanafunzi 12,000 kutoka kila pembe ya dunia.
Vyuo vingine ni Florida, Distance Learning, UMass Online, Boston University, Northeastern University hivi vyote vikiwa ni kutoka nchini Marekani.
Mbali na hivyo, pia kuna vyuo vikuu vya Indiana, Arizona State, Minnesota–Twin Cities, University of Arizona na kile cha Oregon State University–OSU Ecampus.
Vyuo hivi vyote vipo nchini Marekani na moja ya sifa muhimu ambayo imevipa msukumo wa kukaa kwenye nafasi 10 za juu ni kutokana na vyuo kuweza kutambulika na kukubalika kwa zaidi ya asilimia 70 huku wastani wa wanafunzi kuhitimu masomo yao ikiwa ni 68.
Sasa basi, uamuzi ni wako. Amua sasa ili ujiendeleze kielimu.
0 comments:
Post a Comment