Saturday, 21 January 2017

MPAKISTAN ANAYEDAI KUWA NA NGUVU ZAIDI DUNIANI

TANGU vikatuni vya Hulk, jitu la kutisha na lenye nguvu ijapokuwa la kufikirika vilipoanzishwa mapema katika miaka ya 1960, mashabiki wamekuwa wakishangazwa na ushupavu au nguvu zaidi kuliko ghadhabu zake.

Tangu hapo kikatuni hiki kikapata nafasi katika tasnia ya filamu, ambako alizidi kujipatia umaarufu miongoni mwa mashabiki kwa namna alivyo.
Kuanzia hapo wale binadamu halisi wenye nguvu na maumbo makubwa wakajipatia au kujipachika u-Hulk hususani nchini Marekani.
Katika Bara la Asia kulikuwa na Hulk wa Iran na sasa amejitokeza Hulk wa Pakistan, ambaye ndiye makusudio ya makala haya.
Akiwa na uzito wa kilo 436, Arbab Khizer Hayat ameonesha matendo mengi kama vile kusimamisha trekta kwa mikono mitupu.
Pia ana kundi kubwa la wafuasi katika mji wake wa nyumbani wa Mardan, Pakistan.
Arbab Khizer Hayat, maarufu kama Hulk wa Pakistan mwenye umri wa miaka 25 na urefu wa futi 6 na inchi 3 ana ndoto za kuiwakilisha Pakistani katika mchezo wa mieleka wa uzito wa juu unaotambuliwa na Chama cha Mchezo wa Mieleka Duniani (WWE).
Hayat ni mtu mwenye mwili mkubwa, anayehaha kuhakikisha analinda umbo lake hilo la kutisha.
Mieleka na unyanyuzi wa vitu vizito ni mchezo unaopendwa na wengi.
Hata hivyo, linapokuja suala la mtu kudai kuwa na nguvu kuliko wote Pakistan huku akijiaminisha kuwa ni mwenye nguvu dunia bila kuthibitisha hilo, kunashangaza wengi.
Hayat alianza kunenepa katika umri mdogo na akavutiwa na mchezo wa mieleka na kunyanyua vitu vizito na hivyo kujiwa na ndoto ya kuwa mtu mwenye nguvu duniani.
Nilianza kunenepa nikiwa mdogo lakini nilitambua kwamba nahitaji kujiunga na mchezo wa kuinua vitu vizito na kuwa mtu mwenye nguvu duniani. Hivyo, niliendelea kuongeza uzito,” Hayat anasema.
Mnyanyua vitu vizito huyo hivi karibuni alidai kunyanya kilogramu 5000 (tani 5) katika tukio lililofanyika nchini Japan mwaka 2012.
Anadai kutumia zaidi ya kalori 10,000 kwa siku ikiwamo mayai 36 kwa ajili ya kifungua kinywa, kuku wanne, kilo tatu za nyama nyekundu na lita tano za maziwa.
Tajiri huyu kutoka Mardan amekuwa akitukuzwa katika mji wake huo wa nyumbani.
Hata hivyo, watu wengi wanadai kwamba jitu hili linalofanana na hulk ni feki.
Kuna watu wengi duniani wanasema kwamba madai ya Hulk huyu wa Pakistan ni feki na kwamba uhalisia wa video zake unazua maswali mengi.

0 comments:

Post a Comment