Mnyamapori aina
ya faru anayesadikiwa kuwa na umri mkubwa kuliko faru wote duniani, anaishi
katika hifadhi ya Ngorongoro mkoani Arusha.
Faru Fausta
mwenye umri wa miaka 54, ni miongoni mwa faru weusi ambao asili yao ni kusini
mwa Afrika na kutokana na umri mkubwa, kwa sasa amepoteza uwezo wa kuona.
Tofauti na faru
wengine wenye umri mkubwa duniani, kwa mujibu wa vyanzo mbalimbali, Fausta
anaishi katika mazingira ya asili, lakini wengine katika nchi tofauti duniani,
ikiwamo Kenya wanaishi katika mazizi maalumu (zoo) au maeneo yaliyotengwa kwa
faru yajulikanayo kama “Rhino Sanctuary”.
Mhifadhi Mkuu wa
Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA) Dk. Fred Manongi, amesema kwa sasa
Fausta amehifadhiwa katika banda maalumu, baada ya kujeruhiwa na kundi la fisi.
Amesema
wataalamu wa wanyamapori na uhifadhi walikuwa wanatafakari kumwachia kutoka
katika banda hilo, ili arejee na kuishi kwenye mazingira yake ya asili baada ya
afya yake kuimarika.
Kwa upande nchi
jirani ya Kenya Desemba 5 mwaka jana, faru mzee kuliko wote nchini humo
aliyejulikana kwa jina la Solio (42), alifariki dunia.
Faru ni miongoni
mwa wanyamapori ambao wapo katika tishio la kutoweka duniani, kutokana na
majangili kuwaua kisha kuuza pembe zao, soko kubwa likiwa Mashariki ya Mbali.
Kwa mujibu wa
Taasisi ya Save the Rhino ya nchini Uingereza, kulikuwa na faru laki 5 barani
Afrika na Asia mwanzoni mwa karne ya 20, lakini kwa sasa wanakadiriwa kusalia
29,000.
0 comments:
Post a Comment