Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema),kimemtangaza
aliyekuwa Waziri Mkuu wa nchini hiyo Edward Lowassa kuwa mgombea wake wa urais
katika uchaguzi mkuu unaotazamiwa kufanyika tarehe 25 Oktoba mwaka huu.
Mkutano Mkuu wa Chadema uliofanyika jana katika ukumbi wa
Mlimani City jijini Dar es Salaam, umempitisha Lowassa ambaye wiki iliyopita
alikihama chama tawala CCM na kujiunga na chama hicho, kuwa mbeba bendera ya
kugombea urais wa Muungano wa vyama vikuu vya upinzani unaojulikana kama UKAWA.
Muungano huo unajumuisha vyama vya Chadema, CUF, NCCR-Mageuzi
na NLD.
Katika tukio lisilo la kawaida, Makamu Mwenyekiti wa chama
cha CUF Juma Duni Haji ameteuliwa kuwa mgombea mwenza wa urais kwa tiketi ya
Chadema.
Duni amelazimika kuchukua kadi ya uwanachama wa chama hicho
kwa sababu sheria za vyama vya siasa nchini Tanzania haziutambui muungano wa
vyama vya upinzani wa Ukawa kama chama cha siasa.
Wachambuzi wa siasa za Tanzania wamelielezea tukio la leo
kuwa ni changamoto kubwa kwa uchaguzi mkuu wa rais wa mwaka huu unaotazamiwa
kuwa wa aina yake na ambao utakuwa wa tano kufanyika tangu mfumo wa vyama vingi
vya siasa uanzishwe nchini humo mwaka 1992.
Wakati huohuo mgombea
urais kwa tiketi ya CCM John Magufuli, leo alifika ofisi za Tume ya Taifa ya
Uchaguzi (NEC) kuchukua fomu za kugombea wadhifa huo huku akisindikizwa na
umati mkubwa wa wananchi na wafuasi wa chama hicho.
0 comments:
Post a Comment