Friday 29 January 2016

MJI WAFURAHIA MTOTO BAADA YA MIAKA 28..!

Mji mmoja kaskazini mwa Italia, unasherehekea kuzaliwa kwa mtoto wa kwanza tangu mapema miaka ya 1980.

Meya wa mji wa Ostana ulioko eneo lenye vilima la Piedmont, anasema kuzaliwa kwa mtoto huyo ni kutimia kwa ndoto ya jamii ndogo inayoishi katika mji huo.
Idadi ya watu katika mji huo imeshuka sana katika kipindi cha miaka 100 iliyopita, na walikuwa wamesalia watu 84 pekee na ni nusu yao pekee huishi katika mji huo bila kuhamahama Gazeti la La Tampa linasema.
Mtoto Pablo aliyezaliwa katika hospitali moja mjini Turin,amefikisha idadi ya watu mjini humo hadi 85 sasa.
Meya Giacomo Lombardo anasema mji wa Ostana ulikuwa na watu 1,000 mapema miaka ya 1900, lakini wakaanza kupungua baada ya Vita Vikuu vya Pili vya Dunia.
Amesema watu walipungua zaidi kuanzia 1975 ambapo ni watoto 17 pekee waliozaliwa kati ya 1976 na 1987, ambapo mtoto wa mwisho mvulana alizaliwa.
Tangu wakati huo hakuna mtoto mwingine aliyezaliwa hadi sasa mji huo ulipompokea Pablo.
Mji huo unajaribu kukabiliana na hali ya kushuka kwa idadi ya watu, kwa kuunda nafasi za kazi.
Wazazi wa Pablo Silvia na Jose walikuwa wamepanga kuhamia ng’ambo miaka mitano iliyopita, lakini ripoti zinasema waliamua kukaa baada ya kupewa kazi.

Sherehe kubwa imeandaliwa mjini Ostana kusherehekea kuzaliwa kwa Pablo, na kwa mujibu wa La Stampa sanamu ya korongo imewekwa kwenye lango la kuingia mji kwa heshima yake.

0 comments:

Post a Comment