Wednesday 20 January 2016

Walimu marufuku kupaka wanja.!

Serikali wilayani Geita Mkoa wa Geita, imepiga marufuku walimu kuvaa mavazi yasiyolingana na
taaluma yao, na upakaji wanja na rangi ya mdomo kupita kiasi wanapokuwa kazini.
Ofisa Utumishi wa Wilaya ya Geita Thabitha Bugema, alitoa amri hiyo juzi wakati akizungumza na walimu wakuu wa shule za msingi na waratibu elimu, kwenye kikao cha muongozo wa kutumia fedha za elimu bure zilizotolewa na Serikali.
Bugema amesema baadhi ya walimu wanavaa mavazi ya upotoshaji ambayo hayaendani na ya ofisini.
Amesema walimu wa kiume huvaa suruali za jeans, fulana zenye nembo ya timu za mpira na wengine kuvaa mlegezo na kunyoa nywele mitindo isiyo ya heshima.
Amesema kila mtumishi wa Serikali anafahamu mavazi ya ofisini, na kuwataka walimu kubadilika na kuvaa mavazi ya heshima yanayoendana na taaluma yao.
Ofisa Elimu Msingi Wilaya ya Geita Deus Seif, amesema wamepokea Sh80 milioni kwa ajili ya elimu bure na kuwataka wakuu wa shule kuhakikisha zinatumika kama ilivyopangwa.

Mkuu wa wilaya hiyo Manzie Mangochie amewataka walimu na waratibu elimu, kufanya mikutano ya wazazi ya kuwaelimisha maana ya elimu bure na kuwaeleza mambo ambayo Serikali inafanya na wajibu wa wazazi kwa watoto wao. 

0 comments:

Post a Comment