Wednesday 20 January 2016

Radi yaua watu watatu wa familia moja Rufiji

Watu watatu wa familia moja wakazi wa Kijiji cha Mchukwi wilayani Rufiji Mkoa wa
Pwani, wamekufa baada ya kupigwa na radi jikoni wakati mvua zikinyesha jana jioni.
Inadaiwa kuwa radi hiyo ilianza kupiga mti uliokuwa pembezoni mwa jiko hilo kabla ya kuwaua ndugu hao.
Shuhuda wa tukio hilo Amina Tenge ambaye pia ni Ofisa Mtendaji wa kijiji hicho, amesema waliwachukua ndugu hao na kuwapeleka Hospitali ya Misheni ya Mchukwi kwa ajili ya kupatiwa matibabu ya majeraha waliyopata.
Mganga wa zamu wa Hospital hiyo Esther Mtini, amewataja marehemu hao kuwa ni Desteria Simba (40), Deborah Simba (2) na Amani Matimbwa (6).
Akizungumzia ajali hiyo Mkuu wa Wilaya ya Rufiji Nurdin Babu, amewataka wananchi kuepuka kukaa chini ya miti au karibu na miti katika kipindi hiki, ambacho mvua zinaendelea kunyesha kwani ni hatari kwa maisha yao.




Mamlaka ya Hali ya Hewa (TMA), juzi ilitoa tahadhari ya kuwapo kwa mvua kubwa zinazoambatana na radi katika baadhi ya mikoa nchini ukiwamo Pwani.     

0 comments:

Post a Comment