Thursday 13 April 2017

AKAMATWA KWA KUMTALIKI MKEWE KUPITIA KADI YA POSTA.




Mwanamume wa kihindi alikamatwa kwa madai ya unyanyasaji na udanganyifu katika ndoa baada ya kumpa talaka mke wake kwa kumtumia ujumbe kwenye kadi ya posta.

Mohammed Haneef alituma kadi hiyo wiki moja tu baada ya harusi yao, ikiwa na maandishi "talaq" mara tatu kuashiria amempa talaka mkewe.
Mke wake alilalamikia polisi wa kituo cha Hyderabad ambao walisema kuwa ndoa yake na Haneef haikuwa halali kwani hakuwa ametangaza kupewa talaka kwenye ndoa ya awali.
Haneef, mwenye umri wa miaka 38 aliachiliwa kwa dhamana na polisi sasa wanasema watamfungulia shtaka la ubakaji.
"Uchunguzi wetu unaonyesha kuwa utaratibu uliofuatwa kabla wao kuoana sio ule uliofaa kwa sababu hawakuwa na stakabadhi sahihi" naibu kamishna wa polisi V Satyanarayana aliiambia BBC.
"Tunabatilisha dhamana aliyopewa Haneef kwanza kisha tutamkamata na kumshtaki kwa kosa la ubakaji," alisema.
Haneef bado yuko katika ndoa na mkewe wa kwanza. Sheria za kiislamu zinamruhusu mwanamume kuwa na wake hadi nne.
Sheria ya talaka mara tatu ambayo inamkubali mwanamume kumpa talaka mkewe papo hapo inakabiliwa na upinzani mkali nchini India.
Makundi ya akina mama yamekuwa yakiendesha kampeni dhidi ya kitendo hicho na mahakama ya juu zaidi ya India iko katika mchakato wa kuamua kama ni kinyume na katiba.
Wanaharakati wanasema nchi nyingi za Kiislamu, ikiwa ni pamoja na Pakistan na Bangladesh, zimepiga marufuku Talaq mara tatu, lakini bado inatendeka sana nchini India.

0 comments:

Post a Comment