Mbunge wa Jimbo la Kilombero
(Chadema) Peter Lijualikali, amesema licha ya mateso makali aliyoyapata akiwa
gerezani, amefurahia kifungo hicho kwani kimempa heshima kubwa huku akisema ni
kama amepata shahada ya udaktari (Phd).
Lijualikali aliyasema hayo jana muda mfupi baada ya kutoka nje
ya lango la Gereza la Ukonga jijini Dar es Salaam alikokuwa akitumikia kifungo
hicho.
Alielezea hali
ya ubaya wa chakula cha gerezani alitolea mfano wa chakula cha dagaa ambao
iwapo wakioshwa kiwango cha mchanga ni nusu kikombe. “Tulikuwa tunakula ugali
wa dona ambao kwa mtu wa kawaida huwezi kula kwa sababu umechanganywa na
magunzi,” alisema.
Alisema ndani ya
gereza hilo kuna eneo linaitwa Sitaki Shari ambalo hutumika kutesea wafungwa.
Akishuhudia alisema alimwona mfungwa mwenzake ambaye alipigwa katika eneo hilo
kiasi cha kutambaa.
Akizungumzia
uhusiano wake na maofisa wa magereza, alisema kitaasisi ulikuwa ni mbaya japo
kwa askari mmoja mmoja alikuwa akizungumza nao pasipo shida.
Akifafanua alisema
kwa hadhi yake yeye kama mbunge alipaswa kulazwa daraja la tatu ingawa aliwekwa
katika eneo tofauti na kuliacha daraja hilo wakilazwa watoto wa viongozi,
watuhumiwa wa meno ya tembo na raia wa China ambao hakusema walikuwa
wanatuhumiwa kwa kesi gani.
“Magereza kuna
madaraja matatu, la kwanza, pili na la tatu ambalo nilitakiwa kulazwa humo ili
nipewe ulinzi kutokana na hadhi yangu.” Alisema vitendo hivyo na vingine
ambavyo hakuvisema atavipeleka ndani ya Bunge Dodoma.
Awali,
Lijualikali alieleza kile alichokitaja kuwa ni sababu za kifungo hicho akisema
ni msimamo wake wa kukataa Chama Cha Mapinduzi (CCM) kuchakachua kura kwenye
uchaguzi wa Halmashauri ya jimbo hilo.
Alisema msingi
hasa wa kifungo hicho ni uhuni na udhalimu uliofanywa na chama hicho dhidi yake
kwa kuwa kisheria alitakiwa kuruhusiwa kupiga kura kwa maana yeye ni mbunge
halali aliyechaguliwa na wananchi.
Mbali na hilo,
Lijualikali aliwalaumu wale aliowaita kuwa ni wenye hekima kukaa kimya kwa
kitendo kilichomkuta.
0 comments:
Post a Comment